Habari

KQ yafuta barua ya kumtimua Ali Gire

March 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

RICHARD MUNGUTI na IBRAHIM ORUKO

MFANYAKAZI wa Kenya Airways Ali Gire anatarajiwa kurejea kazini leo baada ya shirika hilo – KQ – kufuta barua ya kumtimua kwa kurekodi video ya ndege ikitua Nairobi ikiwa na abiria 239 ikitoka China.

Haya yamebainika Alhamisi katika mahakama jijini Nairobi ambapo maafisa wamemthibitishia Jaji Weldon Korir kwamba hatashtakiwa.

Alikuwa ametimuliwa kwa kurekodi video ya ndege ya China Southern Airlines ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jumatano wiki jana mnamo wakati ambapo virusi vya Corona vinasababisha matatizo ya kiafya kwa watu wengi na vifo kwa wengine.

Corona sasa ikiitwa Covid-19 na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) imesababisha madhara makubwa hasa katika mji wa Wuhan katika Mkoa wa Hubei nchini China.

Mahakama Kuu tayari ilikuwa imewazima maafisa wa usalama dhidi ya ama kumkamata au kumfungulia mashtaka Bw Ali ambaye ni afisa wa usalama JKIA.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Waziri wa Uchukuzi James Macharia kuwaambia wabunge kwamba Ali ni mtu aliyetekeleza uhalifu anayefaa kukumbana na mkono wa sheria.

“Hakuwa mfichua maovu bali mtu anayeweka usalama wa taifa katika hatari kubwa. JKIA ni sehemu maalum ambayo haifai kuanikwa ovyo,” akawaambia wabunge.

Kauli yake iliwakera wabunge waliomlaumu kwa kukosa uwazi, lakini wakamsihi aishawishi KQ imsamehe Bw Ali waliomtaja shujaa aliyefichua ujio wa ndege hiyo.