KTDA yazima mikopo baina ya viwanda na sasa kutegemea benki
SHIRIKA la Maendeleo kuhusu Majani Chai Nchini (KTDA) linafutilia mbali mpango wa mkopo baina ya viwanda ambao umekuwepo kwa miongo mingi na badala yake kugeukia mikopo inayotolewa na benki.
Haya yanajiri kufuatia ufichuzi kuwa viwanda katika eneo la Bonde la Ufa Magharibi vimekopa kutoka viwanda vya Bonde la Ufa Mashariki kitita cha Sh14 bilioni katika miaka iliyopita fedha ambazo hazijalipwa.
Msimamo huo umeafikiwa vilevile baada ya Katibu wa Wizara ya Kilimo, Dkt Paul Kipronoh Ronoh kuagiza Bodi ya Majani Nchini (TBK) inayodhibiti sekta ya majani chai, kukagua mikopo iliyochukuliwa na viwanda vya KTDA.
Mpango huo ulianzishwa ili kuangazia mahitaji ya muda mfupi kifedha na kuwarahisishia mzigo wamiliki mashamba madogo madogo ya majani chai 700,000 wanaouza mazao yao kwa viwanda vya KTDA, unaotokana na athari za mikopo ya muda mfupi na mrefu inayotolewa na benki kufadhili oparesheni za kifedha.
Kufuatia hatua hii, viwanda vyote 71 kuanzia Novemba kati vitaweza kupata mikopo kutoka kwa taasisi za kifedha.
“KTDA ipo kwenye harakati za kufutilia mbali mpango wa kukopeshana baina ya viwanda na mchakato wa kuainisha fedha zilizokopwa awali unaendelea na unakaribia kukamilika ili kuhakikisha uwajibikaji kikamilifu,” ilisema KTDA kupitia taarifa.
Shirika hilo linaruhusu mikopo baina ya viwanda kufadhili gharama za oparesheni hususan ada za stima, ukarabati wa mashine na kufidia uhaba kwenye bonasi wanayolipwa wakulima kila mwaka na viwanda vinavyokumbwa na changamoto za mapato.
“Kuanzia katikati mwezi huu (Novemba), viwanda vitapata ufadhili moja kwa moja kutoka benki kwa riba ya asilimia sita, hatua itakayoboresha uhuru wa kifedha na kuimarisha ustawishaji katika sekta nzima ya majanichai,” walisema wanachama wa Bodi ya KTDA.
Naibu mkurugenzi wa KTDA, Omweno Ombasa, aliwaongoza wakurugenzi wa kimaeneo– Samson Mosonik Menjo, Vincent Arisi, Francis Wanjau na Philiph Langat – kukaribisha wito wa kukagua mikopo kwenye viwanda hivyo.
Hata hivyo, wamesema gharama haipaswi kulimbikiziwa wakuzaji majanichai wanaomiliki mashamba madogo madogo wanaowasilisha mazao yao kwa shirika hilo.
“Kama wanachama wa Bodi ya KTDA, tunataka kusisitiza kuwa hatuna lolote la kuficha na tunakaribisha mchakato wowote wa ukaguzi kisheria unaoimarisha uwazi na uwajibikaji,” walisema wakurugenzi.