Habari

Kumbe ni kelele tu: Utendakazi duni wa wabunge waanikwa

Na EDWIN MUTAI January 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE walipitisha idadi ndogo zaidi ya miswada 49 iliyowasilishwa katika Kikao cha Tatu cha Bunge la Kitaifa, kielelezo cha utendakazi duni wa Bunge la 13.

Bunge hilo ambalo sasa limefikia katikati mwa muhula wake wa miaka mitano, liliweza kupitisha miswada 17 au asilimia 34.6 pekee ya miswada iliyowasilishwa ikilinganishwa na miswada 26 iliyopitishwa katika kipindi sawa na hicho katika Bunge la 12.

Takwimu zilizotolewa Jumanne na Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge zinaonyesha kuwa miswada 17 ilitiwa saini na Rais William Ruto na kuwa sheria.

Kikao cha tatu cha Bunge la 13 kilichoanza Februari 17, 2024 kilitamatika mnamo Desemba 6, mwaka huo.

“Licha ya changamoto ibuka, kikao cha tatu kilifikia haya. Miswada 49 iliwasilishwa bungeni na ni 17 pekee ilitiwa saini. Miswada 19 ya Seneti ilishughulikiwa, Miswada 11 iliyoanzishwa katika Bunge la Kitaifa ilipitishwa na kupitishwa kwa Seneti, Miswada 7 (tano iliyoanzishwa katika Seneti na mbili iliyoanzishwa katika Bunge la Kitaifa) inashughulikiwa katika kamati za upatanishi na miswada iliyosalia iko katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa,” Bw Njoroge akasema.

Bw Njoroge alitoa takwimu hizo siku ya kwanza ya mkutano wa wabunge unaofanyika mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Kati ya masuala mengine, mkutano huo unadurusu hatua ambayo wabunge wamepiga katika utengenezaji wa sheria huku ukiweka msingi wa utendakazi wao katika muda uliosalia wa bunge hili la 13 linalofika kikomo Agosti 9, 2027.

Bw Njoroge alisema kuwa wabunge walishughulikia hoja 161 huku zingine 38 zilikuwa zikisalia kufikia mwisho wa kikao hicho cha tatu, mnamo Desemba 6, 2024.

“Karibu taarifa 312 zimeshughulikiwa baada ya wabunge kuwasilisha ombi huku ripoti 54 za kamati mbalimbali zikijadiliwa na kuidhinishwa na wabunge katika kipindi hicho,” Bw Njoroge akasema.

Karani huyo alisema taratibu za kushughulikiwa kwa miswada zilikumbwa na changamoto kutokana na muda uliotumika wakati wa kushughulikiwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, uliokataliwa.

Muda mwingine ulitumika wakati wa kushughulikiwa kwa hoja ya kumtimua aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi.

Bw Njoroge pia alisema Bunge la Kitaifa liliweza kuidhinisha majina ya watu 85 walioteuliwa na Rais William Ruto kushikilia nyadhifa mbalimbali kuu serikalini, kama Mawaziri, Makatibu wa Wizara, Mwanasheria Mkuu, Inspekta Jenerali na mabalozi wa Kenya katika mataifa mbalimbali.

Karani huyo alisema kuna zaidi ya rasimu 200 za miswada zinazochunguzwa katika hatua mbalimbali katika Kamati kadhaa za Bunge la Kitaifa.

“Katika kikao kijacho, kamati hizo zinatarajiwa kushughulikia rasimu hizi za miswada haraka ili kutoa nafasi kwa wabunge kutekeleza wajibu wake kuwa kujadili,” Bw Njoroge akauambia mkutano huo uliofunguliwa rasmi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Alisema muda wa kuhudumu kwa wanachama wa kamati 18 za bunge unaelekea kukamilika na anasubiri agizo kutoka kwa Spika ili aamuru kuanza cha mchakato wa uteuzi wa wanachama wapya.

Miongoni mwa kamati hizo, kulingana na Bw Njoroge, ni Kamati ya Hadhi na Mamlaka ya Bunge, Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC) na Kamati ya Kughulikia Masilahi ya Wabunge.