Habari

'Kuna wanawake wachache ngazi za uamuzi muhimu miungano ya kutetea wafanyakazi'

September 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

MIUNGANO na mavuguvugu ya kutetea maslahi ya wafanyakazi bado ina idadi ya chini ya wanawake wanaohusika katika utoaji wa uamuzi muhimu nchini, kongamano lajadili.

Hili ni suala ambalo lilijadiliwa Jumanne katika kongamano linaloendelea la Organisation of African Trade Union Unity (OATUU) jijini Nairobi.

Mwenyekiti wa kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini yaani Joint Monitoring and Evaluation Committee, Sudan Kusini, Bw Kalonzo Musyoka alisema kuwa hali hiyo inatia hofu na kuna haja ya kufanya marekebisho upesi.

“Asilimia 30 pekee ya wanawake ndio wana vyeo katika miungano mingi nchini ikiwemo Chama cha Kutetea Walimu nchini Kenya (Knut) na Muungano wa Kutetea Wafanyakazi Nchini (Cotu-K),” alisema Bw Musyoka.

Makamu huyo wa Rais wa zamani ameitaka miungano ya kutetea maslahi ya wafanyikazi kuleta maelewano kati ya waajiri na wafanyakazi ili kudumisha tija.

Amewataka pia wananchi kuheshimu uamuzi na amri za mahakama kila kunapokuwa na mzozo wa kikakazi.

“Tumeshuhudia mara nyingi visa ambapo mahakama inafanya uamuzi ama kutoa amri na upande mmoja unapuuza. Jambo hili si sawa,” akasema Bw Musyoka.