Kura ya maamuzi ifanyike 2022, Duale ashikilia
Na IBRAHIM ORUKO
KIONGOZI wa Wengi Bungeni Aden Duale alisisitiza Jumatatu kuwa mfumo wa bunge ambao utamwezesha Waziri Mkuu kuwa na mamlaka ya juu ndiyo utasaidia kumaliza vurugu ambazo hushuhudiwa kila mara baada ya uchaguzi.
Bw Duale pia alishutumu viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya kwa kupigia debe mfumo wa sasa ambao alisema unabagua jamii ndogo.
Mbunge huyo wa Garissa Mjini, hata hivyo, alisema kwamba hataunga mkono mpango wa kutaka kuandaa kura ya maamuzi kutaka kupanua serikali kwa kuongeza vyeo katika mfumo wa sasa.
Katika mahojiano na Taifa Leo ofisini mwake katika majengo ya Bunge, Bw Duale alisema kwamba swali la kuwataka Wakenya kuamua ikiwa wanataka mfumo wa bunge linafaa kuwasilishwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 ili kupunguza gharama za kuandaa kura ya maamuzi.
Katiba ya 2010 inasema kuwa mfumo wa serikali kubadilishwa ni sharti kuwe na kura ya maamuzi.
“Sitaki kura ya maamuzi ifanyike kabla ya 2022 kwani itasababisha mgawanyiko nchini na hata kukwamisha miradi ya maendeleo ya Rais Uhuru Kenyatta,” akasema Duale.
Kundi la wabunge 39 kutoka eneo la Mlima Kenya Alhamisi lilitishia kukataa ripoti ya jopokazi la BBI, lililobuniwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuandaa ripoti kuhusu namna ya kuunganisha Wakenya, endapo halitashughulikia masilahi ya watu wa ukanda huo.
Walisema eneo la Mlima Kenya halijawakilishwa katika ngazi zote za uongozi ikilinganishwa na idadi ya watu katika maeneo hayo.
“Tunafaa kuwa na idadi ya wawakilishi Bungeni wanaolingana na idadi yetu. Eneo la Mlima Kenya lina idadi kubwa ya watu lakini limewakilishwa na viongozi wachache,” wakasema wabunge hao kupitia taarifa iliyosomwa na mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni.
Zingatio
Jumatatu, Bw Duale alipuuzilia mbali kauli ya wabunge hao huku akisema kuwa Katiba ya Kenya inazingatia idadi ya watu na ukubwa wa eneo.
Alisema kuwa jamii kubwa tano nchini zimekuwa zikikandamiza makabila mengine madogo kwa miaka mingi.
“Ikiwa wao watasisitiza kuwa mtu mmoja, kura moja, watu wa Kaskazini Mashariki pia watasisitiza kuwa kilomita moja iwe na kura moja,” akasema Bw Duale.
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ameonya kuwa hatua ya Bw Duale kuunga mkono BBI ina njama fiche ya kutaka kuvuruga mjadala kuhusu ripoti ya jopokazi.
“Bw Duale hataki ripoti ya BBI na vilevile hapendi mageuzi. Anachofanya Bw Duale ni kutaka kuharibu mjadala kuhusu ripoti ya BBI,” akasema Bw Kuria.
“Bw Duale anadhani kwamba anamsaidia Naibu wa Rais William Ruto lakini ukweli ni kwamba anamharibia,” akaongezea mbunge huyo wa Gatundu Kusini.