Habari

Kutimuliwa kwa Sonko mamlakani kulipangwa Ikulu, shahidi aambia korti

Na RICHARD MUNGUTI July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUONDOLEWA kwa Mike Mbuvi Sonko kama Gavana wa Nairobi kulipangwa katika Ikulu ya Nairobi, Mahakama inayoamua kesi ya ufisadi iliambiwa Jumatatu (Julai 28, 2025).

Aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Gatuzi la Nairobi Bi Winfred Gathangu alifichua haya wakati wa kusikizwa kwa kesi ya ufisadi wa Sh20 milioni dhidi ya Sonko mbele ya hakimu mkazi Charles Ondieki.

Bi Gathangu, mfanyabiashara alisema maafisa wakuu katika Ikulu ya Nairobi mnamo 2019 walimshawishi yeye na maafisa wakuu wenzake katika kaunti ya Nairobi wabuni ushahidi wa uwongo kwa Sonko kuwa alihusika na shughuli za ufisadi.

“Maafisa wakuu kutoka Ikulu ya Nairobi walitushawishi tubuni ushahidi wa ufisadi wa uwongo dhidi ya Sonko kwa lengo la kumtimua mamlakani,” Bi Gathangu alieleza mahakama Jumatatu.

Afisa huyo aliyekuwa akisimamia masuala ya fedha alisema maafisa hao wakuu walimshawishi yeye na maafisa wenzake wawasaidie kubuni ushahidi wa uwongo ndipo kesi za ufisadi zifunguliwe dhidi ya Sonko.

Bi Gathangu alisema maafisa hao kutoka Ikulu walisema “walitaka Sonko afunguliwe kesi za ufisadi ndipo ang’atuliwe mamlakani kwa sababu alikuwa anapambana na ufisadi katika kaunti ya Nairobi.”

Bi Gathangu alisema aliandikisha taarifa mbili katika tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) mnamo Januari 15 na 20 2020 mtawalia.

Aliyekuwa afisa mkuu wa Fedha Kaunti ya Nairobi Winfred Gathangu aliyeambia korti Julai 28, 2025 kwamba maafisa wakuu katika Ikulu ya Nairobi walipanga njama kumng’atua mamlakani Mike Sonko aliyekuwa Gavana wa Nairobi kwa kumsingizia ufisadi. Picha|Richard Munguti

Licha ya kuandika taarifa hizo hakuitwa kutoa ushahidi dhidi ya Sonko.

Alisema baadhi ya mashahidi walioitwa kutoa ushahidi walitoa ushahidi wao faraghani wakihofia maisha yao.

Akijibu swali iwapo Sonko alimshawishi kulipa baadhi ya kampuni na watu wapatao 25,000 waliotoa huduma, Bi Gathangu alisema gavana huyo wa zamani hakumsukuma kulipa wale waliotoa huduma kwa kaunti.

Afisa huyo alisema kile Sonko alifanya ni kulalamika kwamba makeshia katika kaunti ya Nairobi walikuwa wanafanya kazi duni na “alitisha kuwafuta kazi.”

Bi Gathangu alisema baadhi ya makeshia hao walikuwa wamemaliza muda wa zaidi ya miaka mitano; baadhi walitimuliwa kazini na wengine wapya wakaandikwa.

Wakili Assa Nyakundi anayemwakilisha Sonko alimwuliza ikiwa alilipa kampuni ijulikanayo kama JamboPay (Webtribe) pesa kwa huduma za kukusanyia kodi kaunti ya Nairobi.

Akijibu, Bi Gathangu alisema alijua kampuni hiyo ya JamboPay.

Alisema alimfahamu Mkurugenzi wa JamboPay Danson Muchemi akidai kwamba aliahidi kumpa Sonko hongo ya Sh5 milioni kila siku ikiwa atamkubalia kuendelea kutoa huduma kwa kaunti ya Nairobi.

Sonko alimripoti Muchemi kwa polisi kisha maafisa wa polisi wakampa Sonko kifaa cha kurekodi mazugumzo jinsi atakavyopewa hongo na Muchemi.

Wakati wa mjadala baina yao Muchemi alimfichulia Sonko kwamba gavana wa zamani wa Nairobi Evans Kidero aliunda zaidi ya Sh7 bilioni.

Mkanda ulionasa mazugumzo hayo kati ya Sonko na Muchemi ulichezwa kortini kama ushahidi.

Sonko alimrekodi Muchemi alipomtembelea katika makazi ya Kikambala kaunti ya Kilifi.

Kesi inaendelea.