Kwaheri Bob
Na VALENTINE OBARA
“KIFO ni tukio lisiloweza kuepukika! Kwa hivyo nimeamua kutowaza kukihusu kwa sababu hatimaye kitanifikia. Kile nisichofahamu ni lini kitanijia. Nimeamua kujishughulisha na mambo yaliyo muhimu kwangu. Sasa ninajua haiwezekani mtu yeyote kuishi miaka 200,” Bob Collymore, Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom.
Marehemu Collymore alitamka maneno hayo alipohojiwa wakati alipokuwa amelazwa hospitalini nchini Uingereza mwaka 2018.
Bw Collymore, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 61, aliaga dunia Jumatatu asubuhi nyumbani kwake Nairobi kutokana na saratani ya damu.
Aliugua kansa ya damu kwa miaka mingi bila kujua, hadi miaka miwili iliyopita, na imefichuka alikuwa amejiandaa kwa kifo wakati wowote.
Raia huyo wa Uingereza, ambaye ni mzaliwa wa Guyana katika bara la Amerika Kusini, anasindikizwa leo Jumanne katika safari yake ya milele kwenye mazishi ya faragha kabisa.
Alipohojiwa awali, Bw Collymore alieleza kuwa aliugua kwa muda mrefu bila madaktari kufanikiwa kujua kilichokuwa kinamsababishia uchovu, joto jingi mwilini, kutetemeka na maumivu makali hadi mwaka wa 2017 ilipobainika alikuwa na saratani ya damu.
Jumatatu ilifichuka madaktari walikuwa wamemwambia ingekuwa bahati kama angeendelea kuishi baada ya Julai hii, na ikawa kinaya kwake kufariki alfajiri Julai ilipoanza.
Mwanahabari Jeff Koinange, ambaye alikuwa mwandani wa marehemu alisema: “Alikuwa ameambiwa na madaktari wake asifanye mipango yoyote ya miaka mingi ijayo. Aliambiwa itakuwa bahati kama ataishi baada ya Julai, kwa hivyo alijua. Sijawahi kuona yeyote aliyejiandaa kwa kifo kama mwanamume huyu.”
Haya yalithibitishwa na Mwenyekiti wa Safaricom, Bw Nicholas Ng’ang’a, aliyesema mkuu huyo wa kampuni ya mawasiliano iliyo kubwa zaidi nchini, alifariki akiwa mwenye amani moyoni mwake.
“Imekuwa miaka miwili tangu aanze kupokea matibabu, na alifahamu kile alichokuwa anapitia. Alikuwa na amani na alikuwa tayari ndiposa msiba huu ulipotokea alikuwa nyumbani na jamaa zake wa karibu,” akasema kwenye kikao cha wanahabari Nairobi.
Bw Ng’ang’a alisema Bw Collymore alipokea matibabu katika hospitali mbalimbali nchini na ng’ambo, lakini hali yake ikazidi kuwa mbaya katika wiki chache zilizopita.
“Mnamo Oktoba 2017, Bob alienda Uingereza kutibiwa kwa ugonjwa wa Acute Myeloid Leukemia (AML), akarejea nchini Julai 2018 kuendelea na kazi. Amekuwa akitibiwa kwa ugonjwa huu tangu wakati huo katika hospitali mbalimbali, ya mwisho ikiwa Hospitali ya Aga Khan University iliyo Nairobi,” Bw Nganga alisema jana akithibitisha kifo hicho.
Familia
Bw Collymore ameacha mjane, Bi Wambui Kamiru, ambaye walioana Aprili 2, 2016. Alikuwa baba wa watoto wanne.
Marehemu alijiunga na Safaricom mnamo 2010 kuchukua mahali pa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Michael Joseph ambaye alistaafu.
Mnamo Mei mwaka huu, kandarasi yake iliongezwa kwa mwaka mmoja. Hii ilikuwa mara ya pili kwa bodi ya kampuni hiyo kuongeza muda wa kandarasi yake, kwani alipoajiriwa mwaka wa 2010 alitarajiwa kuhudumu kwa miaka mitatu pekee.
Marehemu Collymore alizaliwa 1958, akaanza masomo yake Guyana, Amerika Kusini ambako alikuwa akiishi na nyanyake.
Alihamia Uingereza kuishi na mamake katika mwaka wa 1974 alipofikisha umri wa miaka 16.
Baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Selhurst iliyo Uingereza.
Kabla ya kuajiriwa kusimamia Safaricom, aliwahi kufanya kazi katika shirika la Vodafone, Cellnet, Dixons miongoni mwa mengine.
Maishani mwake, hakuficha jinsi alivyopenda sanaa ya uchoraji, muziki na kuendesha helikopta.