Lazima tuibadilishe Katiba hii – Raila
WYCLIFFE MUIA na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga amependekeza Katiba ifanyiwe mabadiliko ili kubuniwa ngazi tatu za utawala, kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya Katiba ya Bomas.
Akiongea Jumatano katika Kongamano la Ugatuzi mjini Kakamega, Bw Odinga alisema hatua hiyo itafanikisha ugavi sawa wa rasilimali na kufanikisha malengo ya ugatuzi.
Alipendekeza kubuniwa kwa maeneo 14 zaidi ya utawala huku serikali 47 za kaunti zikiendelea kudumishwa kama ilivyo sasa.
“Napendekeza kubuniwa kwa maeneo 14 ya utawala ili kuhakikisha rasilmali zinasambazwa kwa usawa. Maeneo hayo yatasaidiana na serikali 47 za kaunti katika kufanikisha ugatuzi.
Ngazi hizi za utawala zitafanya kazi kwa ushirikiano na Serikali ya kitaifa,” akasema Bw Odinga akiongeza mfumo huo ulipendekezwa katika rasimu ya Bomas.
Baadaye akihutubia wakazi mjini Kakamega, Waziri huyo Mkuu wa zamani alifichua kuwa walikubaliana na Rais Uhuru Kenyatta ‘kubadilisha mambo’ na hakuna kurudi nyuma.
“Kama Raila na Uhuru wamekubaliana kufanya hivyo nani anaweza kupinga?” aliuliza Bw Odinga.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye alikuwa ameandamana na Bw Odinga mjini Kakamega alisema ataongoza kampeni kali wakati ukifika wa kubadilisha katiba.
‘Katiba si mali ya mtu’
“Kuna watu wanafirikia katiba ni mali yao…ikisemekana katiba ibadilishwe nitakuwa mstari wa mbele kushawishi Wakenya kote nchini,” alisema Bw Joho mjini Kakamega baada ya kongamano la magavana.
Naibu Rais William Ruto hata hivyo amekuwa akipinga pendekezo la kubadilisha katiba, haswa kubuni nafasi zaidi serikalini.
Bw Ruto ameahidi kupinga hatua hiyo akisema serikali ya Jubilee kwa sasa imejitolea kutoa huduma kwa wananchi na haina wakati wa kujihusisha na mjadala wa kubadilisha katiba.
Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema chama hicho kinaunga mkono mswada wa mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket lakini akafafanua kuwa haitafaa kumpa waziri mkuu mamlaka yote ya kuendesha serikali bila kumhusisha rais.
“ODM kilikuwa chama cha kwanza kupendekeza kuwepo na mfumo wa uongozi wa nchi kupitia bunge kama ilivyo nchini Uingereza alisema mbunge huyo wa Suba Kusini.
Katika hotuba yake jana, Bw Odinga pia aliwataka magavana kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika vizuri huku akilaani ufisadi uliokithiri katika serikali za kaunti.