Habari

Lenolkulala atakaswa ufisadi, sasa mweupe kama pamba

Na SAM KIPLAGAT November 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Samburu, Bw Moses Lenolkulal, sasa ni mtu huru baada ya Mahakama Kuu kubatilisha kifungo chake cha miaka minane jela na faini ya Sh83.4 milioni.

Bw Lenolkulal alipatikana na hatia yaa kujipatia maslahi ya kibinafsi kupitia kandarasi kati ya serikali ya kaunti na kituo cha mafuta cha Oryx Service Station, lakini alikata rufaa ambayo alishinda.

Mfanyabiashara Hesbon Jack Wachira Ndathi pia aliachiliwa huru baada ya Mahakama Kuu kubatilisha hukumu yake, ikisema hakuna ushahidi uliothibitisha kuwa alikuwa alikuwa ajenti  au mfanyakazi wa Bw Lenolkulal alipokuwa akiendesha kituo hicho cha mafuta.

Katika uamuzi wake, mahakama ilisema hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa wawili hao waligawana faida kutoka kwa biashara hiyo, au kuwa Bw Ndathi alipokea mshahara kutoka Oryx Service Station kama mwakilishi wa Bw Lenolkulal.

“Ni maoni yangu kwamba kipengele cha udhibiti, umiliki na usimamizi wa Oryx hakikuthibitishwa bila shaka yoyote. Hivyo basi, shtaka la mgongano wa maslahi halikuthibitishwa,” ilisema mahakama.

Mahakama ilisisitiza kuwa uamuzi huo haumaanishi kwamba watumishi wa umma wanaruhusiwa kufanya biashara na taasisi wanazotumikia, bali ni kwamba upande wa mashtaka haukuthibitisha uhusiano wa moja kwa moja kati ya Bw Lenolkulal na biashara hiyo ya mafuta.

Mahakama pia ilisema mafuta yaliyosambazwa kwa serikali yalitoka kwa biashara hiyo, lakini ushahidi ulionyesha kuwa Bw Lenolkulal alikuwa amekikodisha kwa Bw Ndathi kwa kodi ya Sh70,000 kwa mwezi, iliyolipwa kila robo mwaka.

Hakukuwa na kipengele katika mkataba kilichoonyesha kuwa wawili hao walikuwa wakigawana faida. Mahakama ilisema kuwa hata kama mahakama ya chini ilihusisha uhusiano wao kama ule wa wakala na bosi, “hakuna kiwango cha tuhuma kinachoweza kuwa msingi wa hukumu bila ushahidi thabiti.”

Mahakama pia ilimuachilia huru aliyekuwa afisa mkuu wa kaunti ya Samburu, Bw Bernard Lesurmat, ikisema hakuna ushahidi uliothibitisha kuwa alihusika katika mchakato wa zabuni ulioruhusu Oryx kusambaza mafuta kwa serikali ya kaunti. Ilibainika kuwa Bw Lesurmat alijiunga na serikali wakati  kituo hicho tayari kilikuwa kimeidhinishwa kufanya biashara na serikali ya kaunti, na jukumu lake lilikuwa tu kuidhinisha malipo ya Sh9 milioni.

Mahakama ilisema kuwa, kwa biashara kusajiliwa kwa jina la mtu hakumaanishi kuwa mtu huyo ndiye anayeidhibiti moja kwa moja. Aidha, ushahidi uliwasilishwa kuonyesha kulikuwa na mkataba kati ya Bw Lenolkulal na Bw Ndathi, na kwamba uhusiano wao haukuwa zaidi ya ule wa mpangaji na mwenye nyumba.

Bw Ndathi alieleza kuwa alichukua mikopo na hata kuuza ardhi kufadhili biashara hiyo baada ya kukodisha kituo, na alitoa stakabadhi za benki kuthibitisha. Mahakama ilikubaliana naye ikisema, “shughuli kama hizo hufanywa na mtu anayechukua hatari binafsi na si mwakilishi wa mtu mwingine.”

Mashahidi pia walithibitisha kuwa serikali ya kaunti ilipokea huduma kamili kwa fedha zilizolipwa Oryx Service Station.