LI PEICHUN: Nakionea Kiswahili fahari
“UKIZUNGUMZA na mtu kwa lugha anayoielewa, hiyo inajikita akilini mwake. Ukizungumza naye kwa lugha yake, hilo linaingia moyoni mwake.”
Nukuu hii ya Nelson Mandela imesikika duniani kote. Ingawa sikuielewa nilipoanza kujifunza Kiswahili baada ya kuwasili Nairobi mwaka wa 2021, sasa inaniongoza kama dira nikijitahidi kuungana na Wakenya.
Kwa nini kujifunza lugha hiyo ya kienyeji ilhali sasa ninaweza kuongea Kiingereza? Kwangu, jibu ni rahisi: Kiswahili kina ‘magic’. Ningezungumza lugha hii na Wakenya, ningezingatiwa kama mmoja wao.
Sikuwa na muda wa kuhudhuria madarasa. Badala yake, nilijifunza kupitia video mtandaoni na kwa msaada wa watu karibu nami: madereva wa kampuni yetu, wanahabari wenzangu, wahudumu wa makazi yangu, na pia marafiki wa Kitanzania mijini Dar es Salaam na Beijing.
Nilichunguza sarufi kwa makini ili kuunda sentensi sahihi – lugha hii ina miundo tofauti kabisa na Kiingereza au Kichina. Kwa mfano, “magari yangu makubwa” ni fomu ya wingi wa “gari kubwa langu” – kila neno linahitaji kubadilika. Tofauti ndogo kama hizi zinaweza kukanganya hata mwanafunzi shupavu.
Bila kukata tamaa, niliendelea. Kwa bahati njema, nimeweza kukumbuka sana licha ya umri wangu wa miaka ya zaidi ya 50. Kiswahili kikawa sehemu ya maisha yangu: mazungumzo na wenyeji, kusikiliza nyimbo kwenye redio, na kusoma habari kwa Kiswahili.
Hatua kwa hatua, nikaanza kujiboresha.
Zaidi ya kuweza kusalimu na kuagiza vitu migahawani, nimetumia Kiswahili katika mazingira rasmi.
Nilialikwa kusimamia sherehe za miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Kenya, nikichanganya Kiswahili, Kiingereza na Kichina.
Katika mahojiano na Rais Paul Kagame wa Rwanda jijini Kigali, nikamuuliza swali kwa Kiswahili – ushindi mdogo ambao ulionyesha juhudi zangu.
Mwaka jana, baada ya kuongoza semina kwa kutumia Kiingereza na Kiswahili, msomi maarufu nchini Kenya, akaniuliza kwa uangalifu: “Bwana Li, kwa nini unajifunza lugha yetu?” Nilipojibu, “Kwa kujifurahisha”, akatikisa kichwa. “Zaidi ya kufurahisha”, akasema, “Ni heshima kwa utamaduni wetu.”
Maneno yake yalinigusa sana. Alikuwa sahihi. Safari yangu haikuwa tu kuhusu lugha – ilikuwa daraja la kufikia roho ya Kenya.
Nimekuja kupenda mila mbalimbali za taifa hili lenye makabila 44: mfumo wa ‘Nyumba Kumi’ unaoimarisha usalama wa jamii na kunikumbusha kamati za vitongoji vya China, ‘Siku ya Kupanda Miti’ ambayo awali niliikosea kama siku ya kukwea miti, na ‘omsherekha’ yaliyotumika na jamii ya Kiluhya kulainisha mboga au nyama ngumu. Kila ugunduzi ulinivutia sana katika utamaduni wa Kenya.
Niliyojifunza yamezaa matunda. Kutoka Nairobi hadi Dar es Salaam, Bujumbura hadi Maputo, wasemaji wa Kiswahili hunisalimu si kama mgeni, bali kama rafiki.
Ukaribu huu unatia nguvu azimio langu la kuendelea na masomo yangu – si tu Kiswahili, bali pia Kikikuyu, Kiluhya na Kijaluo – ili kuelewa vyema jinsi Wakenya wanavyojenga maisha na jamii zao.
Nukuu ya Mandela bado ni sahihi, lakini hapa ndipo inapungukiwa: kuongea kwa moyo, lazima ujaribu kutumia lugha zao, na kuelewa desturi, kanuni na sheria zao.
Kenya imenifundisha kwamba, ili kupata mapenzi na heshima kutoka kwa wenyeji, inabidi ujitahidi kuwasiliana na wao, sentensi kwa sentensi, ‘abusuma kwa abusuma’, ‘muingi kwa muingi’. Wakenya wanaposema “Unasikika kama Mkenya”, wakishikana mikono, nasikia ujumbe usiotamkwa: “Unakaribishwa nyumbani”.
Mwandishi ni Naibu Mkuu wa China Media Group (CMG) barani Afrika