Lori la mafuta ya kupikia lapoteza mwelekeo na kugonga magari Kisii, 2 wafa papo hapo
WATU wawili wamefariki kwenye ajali ya barabarani iliyotokea Jumatano asubuhi katika soko la Daraja Mbili, katika Kaunti ya Kisii.
Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa mbili asubuhi, ilihusisha lori, magari mengine madogo mawili na pikipiki nne.
Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kitutu ya Kati Kazungu Charo, ajali hiyo ilitokea baada ya lori lililokuwa likisafirisha mafuta ya kukaangia kwenye barabara ya Kisii-Kisumu kupoteza mwelekeo.
“Lori hilo lilipoteza mwelekeo na kugonga magari mengine madogo mawili aina ya Prado na Probox. Katika harakati hizo, tuliweza kupoteza maisha ya Wakenya wawili ambao walikuwa wanaendeleza shughuli zao za kibiashara katika eneo hilo,” mkuu huyo wa polisi alisema.
Aliongeza kuwa wendazao walikuwa mwanamume na mwanamke.
Mkuu huyo wa polisi aidha alidokeza kuwa, bodaboda zilizokutanishwa katika ajali hiyo ziliharibika vibaya.
“Watu 11 walipata majeraha na walipelekwa katika hospitali mbali mbali. Wengi wao walikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) kwa matibabu. Watatu kati yao wamo katika hali mbaya lakini tunawaombea wapate kupona ili waweze kuendeleza shughuli za ujenzi wa taifa,” Bw Charo alisema.

Mkuu huyo wa polisi alisema wameanzisha uchunguzi zaidi kubaini kikamilifu jinsi ajali hiyo ilitokea.
Bw Kazungu alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi wa Daraja Mbili, hasa wafanyabiashara wadogo wadogo, wahudumu wa matatu na bodaboda kutoegesha magari au kufanyia biashara zao hadi barabarani.
“Kunakuwanga na soko kubwa eneo hilo lakini ukizuru huko, utapata kuwa wahudumu wa matatu na bodaboda wameegesha magari na pikipiki zao hadi barabarani ilhali hakuna stendi huko. Hivi maajuzi tulifanya hamasisho katika eneo hilo tukiwasihi wenyeji kuhusu usalama wao na tunazidi kutoa wito wasiwe wakifanya biashara zao hadi barabarani ili kuepuka maafa zaidi katika siku zijazo,” Bw kazungu alisema.

Polisi walipata wakati mgumu kuwazuia raia waliofika kwa wingi ajali hiyo ilipotokea wengi wao wakiwa na nia ya kupora mafuta kutoka kwenye lori hilo. Iliwabidi maafisa wa usalama wa kituo cha Nyanchwa kurusha vitoa machozi na kupiga risasi angani ili kuwazubaisha raia hao.
Naibu gavana wa Kisii Elijah Obebo, ambaye alizuru waathiriwa wa ajali hiyo katika hospitali ya Ktrh, alituma risala za rambi rambi kwa ndugu na jamaa za waliopoteza maisha yao.