LSK yajiondoa kutetea mwanablogu ‘aliyejiteka nyara’
CHAMA cha Wanasheria Kenya (LSK) kimewasilisha rasmi ombi la kujiondoa kumwakilisha Kinyagia Ndiangui, kufuatia madai kwamba alifeki kutoweka kwake kwa kujifanya ametekwa nyara.
Awali, LSK ilikuwa imedai kuwa Kinyagia alitekwa nyara na maafisa wa serikali katika mazingira ya kutatanisha na ikaomba korti iagize Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imfikishe kortini.
Hata hivyo, uchunguzi uliofuata ulibaini kuwa Kinyagia alijificha kwa hiari yake mwenyewe, hali iliyodhoofisha uhalali wa kesi nzima.
Katika hati mpya za mahakama, mawakili wa LSK, kampuni ya VR Advocates & Partners LLP, imeomba kuacha kumwakilisha Kinyagia, ikieleza kuwa kuna taarifa zenye utata zinazoharibu uaminifu kati yao.
Katika hati ya kiapo, Wakili Moses Mutungi Kioko alieleza kuwa Kinyagia alitoa taarifa na familia yake ikawasilisha maelezo ambayo ‘yalikuwa tofauti kabisa na ukweli kuhusu jambo hili’.
“Mgongano wa taarifa hizo umefanya iwe vigumu mno kuendelea kumwakilisha,” alisema na kuongeza kuwa juhudi kadhaa za kupata mwafaka kati yao ziligonga mwamba.
Kampuni ya mawakili hiyo imeomba mahakama ruhusa ya kujiondoa kabisa kumwakilisha Kinyagia.
Hata hivyo, Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita alimpa Kinyagia siku 14 kuwasilisha kiapo kinachoeleza sababu ya kutoweka kwake.
Jaji Mwita alipanga kusikiza kesi hiyo Septemba 16, 2025.
Kesi hiyo awali iliibua taharuki kufuatia visa vya watu kutoweka kwa kulazimishwa, lakini udanganyifu wa Kinyagia ulipobainika, sasa umeibua maswali kuhusu matumizi mabaya ya taratibu za kisheria hasa katika masuala nyeti ya kisiasa.
Wiki iliyopita, LSK, ikiwakilishwa na Rais wa chama hicho Faith Odhiambo, iliomba mahakama iwaruhusu kuwahoji Kinyagia Ndiang’ui, binamu yake Lilian Wanjiku Gitonga, na mama yake Margaret Rukwaro.
Bi Odhiambo alisema kuwa kiapo kilichowasilishwa na Gitonga mnamo Julai 3 kilipingana waziwazi na taarifa zilizokuwa zimewasilishwa awali kwa LSK, kabla na baada ya Kinyagia kujitokeza tena kufuatia kutoweka kwake kwa siku 13 bila maelezo.
“Tungependa kuwasilisha ombi kabla ya kusikilizwa kwa kesi hii, likizingatia kiapo kilichoapwa na Bi Lilian Wanjiku Gitonga. Mheshimiwa, kiapo hiki kinakinzana wazi na taarifa tulizopewa awali,” Bi Odhiambo aliambia mahakama.
Rais huyo wa LSK pia alisema chama hicho hakikupewa taarifa yoyote kuhusu kiapo hicho kabla ya kuwasilisha licha ya kuwa kiliwasilisha kesi hiyo.