LSK yapinga pendekezo la Kaluma kwenye mswada wake wa marekebisho ya sheria ya watoto
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha Mawakili Nchini (LSK) kimelitaka Bunge la Kitaifa kutupilia mbali pendekezo la Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma kwamba mahakimu ambao hawako katika ndoa wazimwe kusikiza kesi zinazowahusu watoto.
Rais wa chama hicho Nelson Havi amelitaja pendekezo hilo kama ambalo limepitwa na wakati, linalokwenda kinyume cha Katiba na kuendeleza ubaguzi.
“Bunge halifai kupitisha pendekezo kama hili katika sheria yoyote nchini. Namuomba Rais Uhuru Kenyatta kutotia saini mswada wenye pendekezo potovu kama hili,” akasema Havi.
Pendekezo hilo ambalo wiki jana lilikubaliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Leba na Masilahi ya Kijamii linapendekeza kuifanyia marekebisho sehemu ya 24 ya Sheria ya Watoto ya 2001 ili kutoa nafasi sawa kwa wanaume haki ya kuwatunza watoto waliozaliwa nje ya ndoa.
“Tunahitaji watu (Mahakimu) ambao wamekomaa na wako na familia. Watu ambao wametulia katika maisha ya ndoa na wanaofahamu kuwa maamuzi wanayotoa yanaweza kuvuruga maisha ya watoto,” akasema.
Bw Kaluma alisema baadhi ya maamuzi aliyotaja kama ya “kiajabu” yanatolewa na baadhi ya mahakimu wanaume ambao hawajaoa au wenzao wa kike ambao hawajaolewa.
Bw Kaluma alitoa mfano wa kisa cha Januari 2020 ambapo msichana mwenye umri wa miaka 10 alishangaza Mahakama ya Mwingi alipoangua kilio mara tu hakimu alipoamuru kwamba mamake ndiye mwenye haki ya kumtunza.
“Hii ni wazi kwamba mtoto yule hakukubaliana na uamuzi wa mahakama hiyo ikizingatiwa kuwa amekuwa akiishi na babake baada ya mamake kumtelekeza,” akasema Bw Kaluma.
Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa LSK Mercy Wambua alimtaka Bw Kaluma ambaye pia ni wakili, aondoe pendekezo hilo kwenye mswada wake wa marekebisho ya Sheria ya Watoto 2001.
Bw Kaluma amehusika katika kesi ya muda mrefu na mpenzi wake akitaka apewe haki ya kumtunza mtoto.