Maafisa saba wa polisi wanusurika shambulizi
MAAFISA saba wa polisi katika Kaunti ya Mandera wanauguza majeraha baada ya kunusurika kifo kwa tundu la sindano alfajiri ya Jumanne.
Gari la polisi walilokuwa wakisafiria liliripotiwa kulipuliwa na kilipuzi kilichokuwa kimetegwa barabarani na washukiwa wa kundi la Al-Shabaab.
Tukio hilo lilitokea saa nane alfajiri kwenye barabara ya Rhamu-Mandera kupitia eneo la Khalalio.
Ili kuepuka makabiliano na magaidi, vikosi vya usalama pamoja na watumiaji wengine wa barabara hiyo ya Rhamu-Mandera huamua kupita njia ya Sala kuelekea Mandera mjini kupitia maeneo ya Khalalio na Bela.
“Tunashtuka kwamba magaidi sasa wanaweka vilipuzi hata kwenye njia za kandokando baada ya kutufurusha kutoka barabara kuu ya Rhamu-Mandera,” alisema Bw Adan Shakow, dereva wa matatu.
Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo lilifanyika kati ya Aresa na Gadudia ambapo gari la polisi liliharibiwa vibaya.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Mandera Robinson Ndiwa, alisema kuwa bomu hilo lililipua sehemu ya nyuma ya gari hilo.
“Maafisa wetu walilengwa lakini tunashukuru hakuna aliyejeruhiwa vibaya. Walipata majeraha ya kawaida kwenye misuli na ngozi,” Bw Ndiwa alisema kwa njia ya simu.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, magaidi hao wanashirikiana na wakazi wa eneo hilo kufuatilia mienendo ya maafisa wa usalama.
“Tunahisi magaidi walikuwa na taarifa kuwa maafisa wetu walikuwa wakitumia barabara hiyo, hivyo basi wakaandaa shambulizi. Tuna watu wanaotoa taarifa kwa magaidi kama vile tunavyo kuwa na watoa habari kuhusu mienendo ya magaidi pia,” alieleza.