MAMIA ya waandamanaji Jumanne Julai 8, 2025 walimiminika barabarani mjini Embu wakitaka Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji aachiliwe huru.
Ghasia zilizuka baada ya waandamanaji kuwasha matairi na kushambulia majengo, hali iliyosababisha kufungwa kwa biashara zote kwa siku ya pili mfululizo.
Maandamano yalipoendelea, polisi wa kutuliza ghasia walifika na kujaribu kuwatawanya waandamanaji, lakini walizidiwa nguvu na kulazimika kuomba msaada wa vikosi vya ziada.
Hali ya taharuki ilitanda baada ya waandamanaji kufunga barabara zote kwa mawe na kuwasha moto, hali iliyosababisha usafiri kusimama kabisa mjini humo.
Mji wa Embu, ambao ni mojawapo ya miji yenye shughuli nyingi zaidi katika eneo la Mashariki, ulikwama huku baadhi ya waandamanaji wakionekana wakicheza mpira barabarani.
Mukunji alikamatwa siku ya Jumatatu na maafisa wa upelelezi na kuzuiliwa korokoroni katika kituo cha polisi cha Kibii, Juja, kwa madai ya kuchochea ghasia.
Alikamatwa mchana wakati maandamano ya Saba Saba yakiendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo nyumbani kwake kaunti ya Embu.
Alisajiliwa katika kituo cha polisi cha Kibii chini ya Nambari ya Kitabu cha Matukio (OB) 06/07/07/2025.
Kwa mujibu wa Wakili Ndegwa Njiru, mbunge huyo alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutoka kituo cha polisi cha Juja na kupelekwa Kibii.
Baadaye mbunge huyo alihamishwa hadi mahali pasipojulikana huku wafuasi wake wakishinikiza aachiliwe bila masharti yoyote.
Bw Njiru alisema alipofika Kibii aliambiwa kuwa Mukunji aliachiliwa, lakini akashuku taarifa hizo.
“Kitabu cha OB cha kituo cha Kibii kinaonyesha tu kuwa aliwasili lakini hakijaonyesha kuwa aliachiliwa,” alisema Bw Njiru.
Aliongeza: “OCS alithibitisha kuwa alimsajili kwa madhumuni ya pekee ya kumshikilia.”
Wakili huyo alisema gari la Mbunge huyo bado linazuiliwa katika kituo hicho cha polisi.
Bw Njiru alifichua kuwa afisa wa juu katika kituo hicho alimweleza kuwa Mukunji huenda akafunguliwa mashtaka ya kuchochea ghasia.
Bw Njiru aliandamana na mke wa Mukunji katika kituo hicho.
Wakili huyo alilalamika kuwa polisi walimnyima mke wa Mukunji pamoja na mawakili wanaomhudumia taarifa muhimu kuhusu mteja wao.
Bw Njiru alitoa wito kwa DCI kumfikisha mbunge huyo mahakamani iwapo wana ushahidi kuwa alitenda kosa lolote.
Baadhi ya wakazi wa Embu walilaumu DCI kwa kumtishia Mukunji, wakisema hana hatia.
“Mukunji hakuhusika na maandamano ya Saba Saba na tunataka aachiliwe mara moja,” alisema mmoja wa wakazi.