Habari

Mabaharia 22 wakwama baharini baada ya kutelekezwa na mwajiri wao

Na ANTHONY KITIMO January 17th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WAHUDUMU 22 wa meli ya uvuvi wamekwama katika ufuo wa Pwani Kaunti ya Kilifi kwa zaidi ya siku 15 baada ya mwajiri wao kuwatelekeza.

Wahudumu hao 22 kutoka mataifa mbalimbali wa meli ya uvuvi FV Kivu Spear II wanaishi bila chakula, maji safi na umeme, baada ya jenereta waliyokuwa wakitegemea kuendesha meli hiyo kuharibika siku tano zilizopita.

Meli hiyo iliyosajiliwa nchini Kenya iko na wahudumu 18 kutoka Kenya, mmoja kutoka Indonesia, mmoja kutoka China, mwingine kutoka Tanzania na mwenzao kutoka Pakistani, ambao kwa sasa wanategemea wasamaria wema na wavuvi kupata chakula na maji ili kuendelea kuishi.

Bw Ezekiel Odhiambo, mmoja wa Wakenya walioko ndani ya meli hiyo, alisema hali ni mbaya na kwa sasa wanategemea wasamaria wema kujikimu. “Ni hali mbaya sana, hatuna umeme, chakula wala maji. Nimewahi kukumbana na hali kama hii katika taaluma yangu ya ubaharia, lakini safari hii ni mbaya zaidi kwa kuwa imetokea ndani ya nchi yangu. Tunaomba serikali iingilie kati ili tuweze kulipwa pesa zetu kwani ninadai takriban Sh100, 000,” alisema Bw Odhiambo kupitia simu. Kulingana na wahudumu hao ambao hulipwa kulingana na kazi wanayofanya, wanadai zaidi ya Sh2 milioni kutoka kwa mmiliki aliyewaajiri kufanya uvuvi katika bahari kuu. Msimamazi wa shirika la Mission to Seamen Mombasa, shirika linaloshughilikia maslahi ya wahudumu wa meli, Bw Moses Muli, alisema kuwa wahudumu waliripoti suala hilo kwa Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Usafiri (ITF), ambalo sasa limechukua jukumu la kushughulikia suala hilo.

East Africa Deep Fishing Limited (EADFL) inayohusika na ajira za ubaharia lilithibitisha kuwa wahudumu hao wamekuwa wakiishi bila kulipwa, lakini waliamuwa kusitisha mikataba yao Januari 5 mwaka huu ili kujiondoa rasmi baada ya mmiliki kuwatelekeza.

“Tulikuwa tukimtafuta mmiliki baada ya kubainika kulikuwa na mzozo wa umiliki wa meli, na tukasitisha mikataba ya wahudumu kwa kuwa hatujui mzozo huo utaisha lini. Tumeshirikisha Mamlaka ya Usimamizi wa Masuala ya Bahari Kenya (KMA) na KPA kuhusu suala hili, tukitarajia litapatia suluhisho hivi karibuni,” ilisema EADFL.

Kampuni hiyo ilithibitisha kuwa mishahara ya miezi iliyopita bado haijalipwa na kusema italipwa mara tu mmiliki atakapowasiliana nao.