Habari

Mabasi ya Modern Coast yenye abiria 90 yanaswa Sultan Hamud

December 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

ABIRIA 90 waliokuwa wakisafiri kwa mabasi mawili ya kampuni ya Modern Coast wamekwama mjini Sultan Hamud, kaunti ya Makueni Jumatano alfajiri baada ya polisi kunasa mabasi hayo.

Mabasi hayo yalikuwa yakisafiri kutoka Mombasa kuja maeneo ya bara licha ya marufuku iliyowekwa dhidi yao na Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) wiki jana.

Kila basi lilikuwa na abiria 45 wakati maafisa wa polisi wa trafiki walipoyasimamisha mwendo was aa tisa na nusu alfajiri akasema Kamanda wa Polisi kaunti ya Makueni Joseph Ole Napeiyan,

“Suala hili litashughulikiwa wakati mwingine huku hatua mwafaka zikichukuliwa,” kamanda huyo akaongeza.

Kampuni hiyo ilipokonywa leseni ya kuhudumu baada ya mabasi yake mawili kugongana eneo la Kiogwani katika barabara kuu Mombasa- Nairobi ambapo watu saba walifariki. Watu wengine 60 walijeruhiwa vibaya katika ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa sita za usiku Jumatano wiki jana.

Kila moja ya mabasi yaliyonaswa yalikuwa na abiria 45 wakati maafisa wa polisi wa trafiki walipoyasimamisha katika kizuizi cha barabara mjini Sultan Hamud.

Mnamo Jumanne kulichipuza habari za kukanganya kwamba NTSA imeondoa marufuku dhidi ya kampuni hiyo ya Modern Coast na kuhusu mabasi yake kurejelea huduma.

Hata hivyo mamlaka hiyo ilikana madai hayo.

“Tungependa kujulisha umma kwamba marufuku dhidi ya mabasi ya Modern Coast Express haijaondolewa. Habari zinazoenezwa kwamba NTSA imeondoa marufuku hiyo ni za uwongo,” ikasema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Awali kampuni hiyo ilikuwa imesema kwamba NTSA imeirejeshea leseni ya kuhudumu baada ya kukagua mabasi yake.

“Ni furaha yetu kuwajulisha wateja wetu kwamba tumepata ruhusa kutoka kwa NTSA kwamba turejelea shughuli zetu za kawaida kuanzia saa saba mchana.. Desemba 17,” ujumbe huo ukasema.

Baadaye kampuni hiyo iliwatumia jumbe fupi wateja wake kwamba mabasi hayo yangeanza safari saa saba za mchana Jumanne.