Mabroka watatu kuhukumiwa kwa ulaghai wa Sh1.6 milioni
MABROKA watatu Jumanne waliwekwa kizuizini kwa kumlaghai Mfanyabiashara wa mafuta Mary Waruguru Ngugi Sh1.6 milioni.
Josephat Mogwambo Nyamwange almaarufu Ben, Evans Mogeni Ondari anayefahamika kama Patrick na Ben Nyabuga Ochoki, wanaendelea kuzuiliwa kwenye Kituo cha Capitol Hill, Nairobi wakisubiri kuangushiwa hukumu Alhamisi wiki hii.
Hakimu Mwandamizi Mahakama ya Milimani Benmark Ekhubi aliwapata na hatia ya wizi, kughushi barua za tenda za mafuta na kujifanya wafanyakazi wa lililokuwa Shirika la Kutoa Huduma za Jiji (NMS).
Pia walipatikana na hatia ya kujaribu kumwibia Bi Waruguru mitungi 250 ya lita 20 ya mafuta ya kupikia ya Rina. Mafuta hayo ni thamani ya Sh2,146,000 katika Hoteli ya Pronto jijini Nairobi.
Washtakiwa hao walijitengenezea cheti cha mauzo ya mafuta hayo wakidai stakabadhi hiyo ilikuwa imeandaliwa na NMS.
Walimkabidhi Bi Waruguru cheti hicho wakidai wamekubaliwa kuuzia Kampuni ya Mount Olive mitungi 400 za lita 20 za mafuta ya Rina. Shtaka lilisema walikuwa wanajua wanamdanganya Bi Waruguru na wakaishia kumhadaa.