Mabwanyenye wa SHA kuanza kufyonza mabilioni kila mwezi licha ya kesi kortini
WAZIRI wa Afya Aden Duale amechapisha kanuni mpya za kidijitali zinazofungua mwanya kwa muungano unaoongozwa na Safaricom PLC kuanza kupokea mamilioni ya pesa kila mwezi kama sehemu ya kurejesha uwekezaji wao wa Sh104 bilioni katika mfumo wa afya unaohusishwa na mpango wa Rais William Ruto wa huduma ya afya kwa wote, SHA.
Mnamo Aprili 9, Bw Duale alichapisha kanuni mbili kuu: moja kuhusu ubadilishanaji wa data na nyingine kuhusu usimamizi wa taarifa za afya, ambazo zinasawazisha mfumo huo mpya na kuweka msingi wa malipo kwa Safaricom na washirika wake huku kesi mahakamani kupinga kandarasi hiyo ikiendelea.
Kanuni hizo zinatambua vipengele muhimu vya mfumo huo, kama vile sajili za wagonjwa na madai ya bima, huduma za tiba kwa njia ya mtandao na mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa afya.
“Lengo la kanuni hizi ni kuanzisha na kutekeleza sehemu ya ubadilishanaji wa data na kuhakikisha usimamizi salama wa taarifa za afya kupitia programu na teknolojia za afya mtandaoni,” alisema Bw Duale.
Kulingana na kandarasi iliyotiwa saini Agosti 9, 2024, muungano wa Safaricom ulitarajiwa kuanza kupokea Sh500 milioni kila mwezi kuanzia Februari 2025, kiasi ambacho kingepanda mwaka 2026 hadi Sh650 milioni, Sh900 milioni mwaka 2027, na Sh1.065 bilioni kati ya 2028 hadi 2032.
Mnamo 2033 malipo yangeshuka hadi Sh1 bilioni, kisha Sh900 milioni kati ya Januari hadi Aprili 2034, kabla ya malipo ya mwisho ya Sh500 milioni mwezi Juni 2034.
Malipo haya yote yanategemea kufanikishwa kwa hatua maalum za mradi lakini Bw Duale alisema hadi sasa hakuna fedha zilizolipwa, dalili kwamba muungano huo bado haujakamilisha vipengele muhimu vya utekelezaji.
Seneta wa Busia Okiya Omtatah alipinga utekelezaji wa mradi huo mahakamani, akidai kuwa mfumo huo utabakia kuwa mali ya Safaricom hata baada ya kulipwa mabilioni hayo.
Omtatah pia alisema kuwa shirika sahihi la kushughulikia ununuzi huo lilipaswa kuwa Mamlaka ya Afya (DHA), na si Wizara ya Afya. Aidha, alidai Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) ulianzishwa bila sheria za kuusimamia.
Safaricom na washirika wake walijibu wakisisitiza kuwa mchakato wa ununuzi ulifuata sheria, na kwamba aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alitoa kibali rasmi kwa kandarasi hiyo.
Wizara ya Afya ilijitetea kwa kusema kuwa kesi ya Omtatah sio ya kikatiba, bali ni mgogoro wa zabuni, na hivyo haikufaa kufunguliwa katika mahakama ya katiba.
Kampuni mbalimbali zilisajiliwa kuwakilisha maslahi ya Apeiro nchini Kenya, lakini yalisambaratishwa mwishoni mwa 2024.
Mnamo Julai 5, 2024, kampuni ya Apeiro Kenya Technologies Ltd ilisajiliwa nchini Kenya ikiwa na SIH Africa Ltd kama mmiliki pekee.
Watu wafuatao waliorodheshwa kama wakurugenzi wa kampuni hiyo, lakini hawakuwa na hisa zozote: Inder Deep Singh Virdi, Judy Mwende Gatabaki, Rufus Maina, Aswanth Bindhu Lambodaran.
Muungano huo pia unashirikisha Safaricom PLC (serikali ya Kenya na Vodacom ya Afrika Kusini kila moja inamiliki asilimia 35, huku Vodafone UK ikiwa na asilimia) Apeiro Ltd (kampuni ya UAE inayoongozwa na kampuni kubwa ya uwekezaji duniani – IHC), Konvergenz Network Solutions (kampuni ya Kenya, ambayo asilimia 90 inamilikiwa na Konvergenz Holding Co.)
Watu binafsi na mawakili pia wametajwa kama wamiliki au wenyehisa wa kampuni zinazohusika, ikiwa ni pamoja na kampuni za Kenya kama Galva Investments, Commtech Consortium, na Pitfield Auto Ltd.