Habari

Macharia ashikilia SGR ni mradi wa faida kwa uchumi wa nchi

August 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Uchukuzi, Barabara na Ujenzi, Dkt James Macharia amesema Jumatano kwamba mtambo wa reli ya kisasa (SGR) una biashara ya faida ya Sh400 milioni.

Amesema kuwa kwa mwezi mtambo huo unaingiza biashara ya Sh2.2 bilioni huku gharama zikiwa ni Sh1.82 bilioni hivyo basi kushikilia kuwa hiyo ni hesabu ya faida.

Akiwa katika Kaunti ya Murang’a, waziri Macharia amesema mtambo huo una faida tele katika uchukuzi wa abiria na unatarajiwa kuzidisha faida hiyo wakati biashara ya uchukuzi wa mizigo itashika kasi kutokana na mikataba ya ushirika na wadau katika biashara ya uchukuzi.

Amepuuza madai kuwa kwa sasa SGR ni mradi wa hasara.

Macharia amesema mradi huo wa SGR ndiyo ‘mtamu’ zaidi utawala wa Mwai Kibaki uliweka kwa ratiba ya utekelezaji mwaka wa 2013 na ambapo mwaka wa 2014 serikali ya Uhuru Kenyatta ilitoa mkataba rasmi wa kibiashara kuuhusu.

Amesema mkataba huo ulifuatiwa na mwingine kwa kasi wa ufadhili na bajeti ikaandaliwa.

“Kuanzia 2015, tulianza kutekeleza mradi huo na katika kipindi cha miaka miwili, ukafanikishwa na hesabu zote za kina zinaonyesha kuwa uchumi unavuna faida tele,” akasema.

Amesema kuwa kuna wenye nia mbaya kwa uchumi ambao wanatumia kila utapeli wa ithibati kuudunisha.

“Hufai kupinga mradi kama huo kwa msingi wa kujitakasa kama uliye na umakinifu wa kiuchumi. Weledi wako wa kiuchumi ikiwa ni wa kusambaza mahangaiko na kuvunja watu moyo, basi unafaa tu kutangaza rasmi kuwa huufai ulimwengu kwa lolote. Utaonekana mjinga machoni mwa wale wanaonufaika,” akasema.

Ameongeza kuwa kwa sasa mtambo huo uko katika mkondo sawa wa kibiashara na hakuna shaka yoyote kuwa ni mradi wa manufaa halisi kwa uchumi wa taifa.

“Na kwa kuwa tunaendelea mbele na kujenga mkondo wa kuelekea hadi Naivasha, katika siku za usoni, faida kutoka uchukuzi wa reli itakuwa ya umuhimu mkubwa katika uchumi wa kimaeneo na kitaifa,” amesema.

Pato

Amefafanua kwamba katika kipindi cha mwaka wa kifedha wa 2019/20, ukadiriaji ni kuwa pato kwa mwezi kutoka huduma za SGR litakuwa Sh3.3 bilioni.

“Kabla ya mwaka wa 2022, faida pekee kutoka SGR itakuwa zaidi ya Sh5 bilioni. Walio na ufahamu wa hesabu za uwekezaji watakiri kuwa faida hupanuliwa katika kipindi fulani cha utendakazi. Kwa sasa, mtambo huu wetu uko katika mkondo huo wa upanuzi na utaimarika hadi kuwa wa kuwa kiungo thabiti cha pato kwa uchumi kwa taifa,” akasema.

Amesema kuwa cha maana zaidi ni kuona jinsi mtambo huo umechochea shughuli za kiuchumi katika maeneo ambayo umepitia, huku kukichipuka biashara za kuwaajiri wengi katika maeneo ambayo “yalikuwa yamesahaulika.”

Kwa mtazamo wake ni kwamba gharama ya kujenga SGR ya Sh327 bilioni haikuwa ya juu kama inavyodaiwa na wengi akisema kuwa fidia kwa wamiliki wa mashamba ndiyo ilizidisha kiwango hicho.

Amesema serikali haingetwaa vipande vya ardhi vya watu kwa mabavu bila ya kuwafidia kwa kuwa kufanya hivyo kungekuwa sawa na utapeli wa kiutawala.