Mackenzie alivyovuruga akili ya waumini kabla ya kuwaua
Kiini cha mkasa huo kilikuwa mhubiri Paul Mackenzie, aliyeaminisha wafuasi wake kuwa kufunga hadi kufa kungewasaidia kukutana na Yesu.
Mackenzie alianzisha kanisa la Good News International (GNI) mnamo 2003 ila likasajiliwa rasmi mnamo 2010. Mnamo 2012, huduma hiyo ilisajili kampuni ya Good News Media (K) Limited, iliyoendesha kituo cha televisheni cha Times TV mjini Malindi.
Kwa miaka mingi, shughuli zake ziliibua wasiwasi kuhusu itikadi kali, elimu ya watoto na kukataa matibabu ya kisasa. Wafuasi waliitwa Wateule na kufundishwa kuachana na mali za dunia, huku serikali ikisawiriwa kama adui.
Mnamo 2017, Mackenzie alikabiliwa na mashtaka yaliyohusiana na kueneza itikadi kali na kuendesha taasisi ya elimu isiyosajiliwa. Katika kesi moja, aliachiliwa baada ya makubaliano na upande wa mashtaka na kuamriwa kudumisha tabia njema.
Katika kesi nyingine, aliachiliwa kwa dhamana na hatimaye akaachiliwa huru mnamo 2021.
Mnamo mwaka huo huo, watoto 43 wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na 13 waliokolewa kutoka katika majengo ya GNI eneo la Mayungu. Ripoti zilisema baadhi yao walizuiliwa, kunyimwa elimu na kufundishwa dini.
Mahakama iliagiza wapate ushauri nasaha na matibabu kabla ya kurejeshwa kwa familia zao.
Mnamo 2019, Kamati ya raia wa Mahakama ya Kaunti ya Kilifi ilijadili malalamishi kuhusu kuenezwa kwa itikadi kali kwa watoto kupitia kanisa na televisheni ya Mackenzie. Mamlaka ya Mawasiliano baadaye ilifuta leseni ya Times TV.
Mackenzie pia alishtakiwa kwa kusambaza filamu zisizokaguliwa na kuendesha studio bila leseni. Mnamo Novemba 10, 2023, alipatikana na hatia ya makosa hayo na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi sita, lakini akaachiliwa huru kuhusu shtaka la kuchochea watu kukiuka sheria.
Wakati huo, baadhi ya wafuasi wake walikuwa wameanza kuhamia Shakahola mnamo 2019, huku idadi ikiongezeka wakati wa janga la Corona.
Upande wa mashtaka ulisema walifundishwa kufunga hadi kufa ili waende mbinguni, huku watoto wakitarajiwa kufa kwanza, wakifuatiwa na wanawake kisha wanaume.
Mackenzie na washukiwa wenzake 30 baadaye walishtakiwa kwa mauaji ya watoto 191. Wote walikana mashtaka.
Mahakama Kuu ya Malindi iliamuru mnamo 2024 mashtaka hayo yapunguzwe yasizidi 12, lakini Mahakama ya Rufaa ilirejesha mashtaka yote 191 Aprili 11, 2025.
Kesi ilianza kusikilizwa Agosti mwaka jana baada ya mvutano wa kisheria, na hukumu ikatolewa katika Mahakama Kuu ya Mombasa Jumatatu.
Baada ya mkasa huo kufichuliwa, JSC ilisema ingechunguza jinsi kesi za awali za Mackenzie zilivyoshughulikiwa ili kubaini iwapo kulikuwa na mapungufu katika utoaji wa haki.
Mkasa wa Shakahola umeibua maswali kuhusu jinsi mamlaka zilivyoshughulikia tahadhari kadhaa za awali na iwapo kuchukuliwa kwa hatua za mapema zingeweza kuzuia vifo hivyo.