Madai ya hongo hapa na pale chaguzi ndogo zikiendelea
CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) na Muungano wa Upinzani zilidai Alhamisi kwamba kulikuwa na utoaji hongo wa wazi kwa wapigakura wakati wa uchaguzi mdogo wa Mbeere North, huku zoezi hilo likiendelea chini ya ulinzi mkali.
Hayo yalijiri huku UDA na vyama vya upinzani vikiweka mikakati ya kulinda kura yao dhidi ya wizi na udanganyifu.
Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi, mgombeaji wa UDA Leonard Muthende na Duncan Mbui wa Chama cha Kazi (CCK) walidai kwamba wapigakura walikuwa wakihongwa hadharani katika maeneo kadhaa.
“Tumeona mambo haya sehemu nyingi. Tunaomba IEBC iwe makini ili kuhakikisha uchaguzi ni wa kuaminika,” alisema Bw Muthende.
Bw Ruku na Bw Muturi walirushiana lawama, kila mmoja akimlaumu mwingine kwa kuwahonga wapigakura na kuchochea vurugu zilizoshuhudiwa katika baadhi ya vituo.
Bw Ruku alirejelea kisa cha mtafaruku katika kituo cha kupigia kura cha Siakago Hall ambapo Bw Muturi na wafuasi wake waliwavamia watu wawili waliodaiwa kuvaa mavazi yenye rangi zinazohusishwa na vyama vya kisiasa.
Bw Muturi alimuona mmoja wao akiwa na fulana ya njano na kumvuta hadi nje ya kituo. Akiungwa mkono na wafuasi wake, alimwamuru aondoke.
Bw Muturi alimkamata mwanaume mwingine aliyekuwa amevaa jaketi jekundu na, kwa kushirikiana na wafuasi wake, wakamtoa nje wakimlaumu kuwa mfuasi wa UDA aliyekuwa akijaribu kushawishi wapigakura.

Mvutano uliongezeka eneo hilo huku watu hao wakitoroka kituo cha kupigia kura.
Mapema alfajiri, zoezi la upigaji kura lilianza saa kumi na mbili asubuhi katika Shule ya Msingi ya Kanyuambora Low Cost Boarding na Kiathambu, licha ya madai ya hongo yaliyotolewa na pande zote mbili—UDA na upinzani.
Katika Kiathambu, mgombea wa CCK Duncan Mbui alidai kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki kutokana na vitisho na vitendo vya kuhonga wapigakura.
Zoezi la kulinda kura pia lilionekana kukita mizizi, pande zote mbili zikipeleka maajenti katika kila kituo, huku baadhi yao wakiorodhesha majina ya wapigakura waliowasili.
Novemba 25, 2025, Naibu Rais Kithure Kindiki alifanya mikutano na maajenti na maafisa wengine na kuwataka wahamasishe wapigakura wajitokeze.
Bw Muturi alisisitiza kuwa hawataruhusu kura zao “kuibwa”.
“Tunataka kuwaambia wafuasi wetu kuwa kila kura itahesabiwa. Hatutatishwa na yeyote, na tutahakikisha kura za mgombea wetu ziko salama,” alisema Bw Muturi.