Habari

Madai ya mauaji: Wanajua nini?

July 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA na WANDERI KAMAU

MATAMSHI ya washirika wa Naibu Rais William Ruto kuhusu dai la njama za kumuua yameibua maswali kuhusu wanayofahamu na kwa nini hawataki kuwasilisha ushahidi walio nao kwa wapelelezi ili usaidie katika uchunguzi.

Kufikia sasa, wanasiasa wanaounga Dkt Ruto katika kundi maarufu la ‘Tangatanga’ wametoa kauli ambazo zinaonyesha huenda wako na habari kuhusu madai hayo.

Madai ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Dijitali katika Ikulu, Bw Dennis Itumbi kwamba, ana video kuhusu mikutano ya kupanga njama hizo pia yanaibua maswali kuhusu anayofahamu na kwa nini hakujitolea kupasha polisi kabla ya kukamatwa.

Bw Itumbi alikamatwa mnamo Jumatano na makachero wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) jijini Nairobi kwa tuhuma za kuandika barua iliyodai mawaziri kadhaa walipanga kumuua Dkt Ruto.

Anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga kwa siku tano uchunguzi ukiendelea.

Kukamatwa kwake kuliwafanya wanasiasa wanaomuunga Naibu Rais kuchemka kwa hasira na kumlaumu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti.

Kuwafanya watu kusahau

Kulingana na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kukamatwa kwa Bw Itumbi kulilenga kufanya watu wasahau mkutano ambao mawaziri kadhaa wanadaiwa kupanga njama za kumuua Dkt Ruto.

Haieleweki alivyofahamu kwamba wapelelezi walitaka kuzima uchunguzi kuhusu njama hizo.

Wapelelezi walisema hawakuweza kuchunguza madai ya mauaji dhidi ya Dkt Ruto kwa sababu hakuandikisha taarifa na wakaamua kuchunguza barua iliyosambazwa mitandaoni ikieleza baadhi ya mawaziri walihusika.

Mawaziri waliotajwa ni Joe Mucheru (Habari na Mawasiliano), Peter Munya (Viwanda), Sicily Kariuki (Afya) na James Macharia (Uchukuzi). Wamekanusha madai hayo wakisema kwamba, walikutana kujadili miradi ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya.

Wandani wa karibu wa Dkt Ruto wamenukuliwa wakisema kuwa, wana ushahidi ambao utafichua njama hizo ambao hawataki kuuwasilisha kwa wapelelezi inavyohitajika.

Kulingana na Mbunge wa Soi, Caleb Kositany, wale ambao wanapuuzilia mbali madai hayo watapata mshangao katika siku kadhaa zijazo.

“Video na kanda za sauti tulizo nazo zina ushahidi wa kutosha. Njama hiyo inapaswa kusuluhishwa kabla ya mauaji halisi kufanyika,” alisema kuashiria kwamba kuna habari wandani wa Ruto wanazobana zinazoweza kusaidia katika uchunguzi

Naye Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa alionya kuwa baadhi ya maafisa wakuu serikalini wanatumia nyadhifa zao kuwatisha watu kutokana na miegemeo yao ya kisiasa.

“Imekuwa kawaida kwa kila mmoja anayehusiana na Dkt Ruto kuonekana kama mhalifu ama kuhusishwa na uhalifu,” alisema.

Wakizungumza katika Kaunti ya Busia mnamo Ijumaa, baadhi ya wabunge kutoka eneo la Magharibi waliomba DCI kufanya juhudi kamili kubaini ukweli kuhusu njama hizo, badala ya kuwakamata watu tu, ili kuwafumba macho Wakenya kuhusu ukweli wa madai hayo.

Wabunge Didmus Barasa (Kimilili), Geoffrey Omuse (Teso Kusini), Janet Nangabo (Trans Nzoia), John Waluke (Sirisia), Mwambu Mabonga (Bumula) na James Mukwe (Kabuchai) walieleza ghadhabu yao kuhusu namna Mkurugenzi wa DCI, Bw George Kinoti anavyoendesha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Wabunge hao walisema kukamatwa kwa Bw Itumbi ni njama za kuzuia ukweli kamili kuhusu mpango wa mkutano huo, unaodaiwa kufanyika katika hoteli ya La Mada jijini Nairobi.

Walisema lazima uchunguzi ubaini lengo la mkutano huo, lakini si mwandishi wa barua hiyo ambayo inachunguzwa ikiwa ni ‘feki’.