Madereva wapewa tahadhari msimu wa sherehe ukiwadia
WASIMAMIZI wa sekta ya uchukuzi wa umma (PSV) wametoa tahadhari kwa wahudumu kuzingatia sheria ili kudhibiti ongezeko la ajali za barabarani, huku wananchi wengi wakianza safari kwa ajili ya sherehe za Desemba.
Chama cha wamiliki wa matatu kinasema ajali husababishwa na madereva wanaolazimishwa kufanya kazi kupita kiasi au magari yasiyofanyiwa ukarabati muhimu.
Naibu Rais wa Pili wa chama hicho, Bw Salim Mbarak, alisema sekta ya matatu inahitaji nidhamu ya haraka na utekelezaji wa kanuni ili kuzuia vifo vinavyojitokeza kipindi hiki.
“Huu ndio msimu wenye msongamano mkubwa. Wanachama wetu wahakikishe magari yamekaguliwa na yako salama barabarani,” alisema katika mahojiano.
Alionya kuwa, magari ya safari za mijini hayatakiwi kutumiwa kwa safari za masafa marefu kwa sababu kufanya hivyo ni hatari na hakukubaliki kisheria.
Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama na Uchukuzi (NTSA), vifo vya watu 4,748 vilinakiliwa mwaka uliopita kutokana na ajali barabarani.
Ajali hizo zilichangiwa na uchovu, mwendo wa kasi na hitilafu za mitambo kwenye magari. Bw Mbarak alisema takwimu hizo zinapaswa kuwa onyo kwa wahudumu wanaopuuzia viwango vya usalama.
“Hitilafu za magari na ukosefu wa ukarabati zinaendelea kuua abiria. Kila matatu lazima ikaguliwe kabla ya safari,” alisema.
Aliitaka NTSA kushirikiana kwa karibu na polisi wa trafiki kwenye barabara kuu za Mombasa–Nairobi, Nairobi–Eldoret na Nairobi–Kisumu ili kuondoa magari mabovu na kuwakamata madereva wanaosababisha hatari.
“Mwendokasi bado ni janga. Madereva hukimbizana kutafuta faida, lakini hasara yake huwa maisha ya watu,” alisema.
Aliongeza kuwa, baadhi ya madereva na makanga hutumia pombe au dawa za kulevya wakiwa kazini, tabia aliyoitaja kuwa uhalifu unaoweza kuua abiria wote. Alihimiza mashirika ya usalama kuongeza ukaguzi wa ulevi barabarani.
Bw Mbarak alisema alama duni za barabarani zinachangia ajali, hasa katika maeneo yenye vizuizi, mteremko au njia za wanyama.
Aliitaka serikali kuu na za kaunti kuhakikisha alama zinaonekana hata usiku. Aliongeza kuwa, uchovu wa madereva umeendelea kuwa tishio katika safari ndefu, wengi wakilazimishwa kufanya safari mfululizo bila kupumzika.
“Uchovu hupunguza umakini na mwitikio wa haraka. Ni hatari kama ulevi,” alisema.
Alisema abiria wana jukumu muhimu kupunguza ajali kwa kukataa kupanda magari yaliyobeba kupita kiasi na kuripoti madereva wanaoendesha kiholela. “Sauti ya abiria inaweza kuokoa maisha,” alisema.
Chama kilisema kitaendelea kuelimisha wanachama kuhusu urekebishaji wa magari na nidhamu barabarani.