Madiwani wa UDA Nairobi wataka mwelekeo baada ya Sakaja kuguria ODM
BAADHI ya madiwani na wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali katika Kaunti ya Nairobi kupitia UDA wameutaka uongozi wa chama hicho kutoa mwelekeo kuhusu mustakabali wao wa kisiasa kufuatia hatua ya Gavana Johnson Sakaja kujiunga na ODM hivi majuzi.
Wakiongozwa na Diwani Mteule Cecilia Wairimu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya UDA, walisema uongozi wa chama unapaswa kushughulikia hali ya sintofahamu inayowakabili wagombeaji wake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Wamedai kuwa wakati washirika wao wa ODM katika Serikali Jumuishi wanaendelea kupokea wanachama wapya, kubadilisha mikakati na kuwavutia viongozi wengine huku maafisa wa ngazi za juu wa UDA wameendelea kunyamaza.
Pia wametaka wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali waruhusiwe kufanya kampeni bila kusumbuliwa na kuonya dhidi ya mpango wa kugawana maeneo ya kisiasa (zoning) jijini Nairobi.
“Kama UDA, tutakuwa na wagombeaji wa ugavana, mwakilishi wa wanawake, useneta, ubunge na uwakilishi wa wadi. Hatutabadilisha msimamo wetu. Watu wanapaswa kujua kuwa UDA ni chama cha Rais William Ruto na ana mipango yake. Akizungumza, watu watashangaa,” akasema Bi Wairimu.
Alisisitiza kuwa hatua ya Bw Sakaja kuhamia ODM haitavuruga mipango ya UDA ya kujiimarisha katika maeneobunge yote 17 ya Nairobi kabla ya uchaguzi wa 2027.
Alitaja hatua ya gavana huyo kuwa dharau kwa chama kilichomdhamini kuwania ugavana 2022 na kumuunga mkono wakati alipokabiliwa na jaribio la kung’atuliwa mamlakani.
Kiongozi wa vijana Triza Miroya alisema UDA bado ina nguvu Nairobi licha ya kile alichokitaja kuwa propaganda zinazosambazwa mitandaoni.
Aliongeza kuwa vijana wamenufaika na utawala wa sasa kupitia uundaji wa nafasi za ajira na mfumo mpya wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu.
“Tunaendelea kuwa imara mashinani na UDA inazidi kuimarika,” akasema Bi Miroya.
Naye Diwani Mteule Virginia Waitherero alisema ajenda ya Rais Ruto iko wazi na wataendelea kuunga mkono azma yake ya kuchaguliwa tena.
Alisema watawaunga mkono wagombeaji wa UDA kuhakikisha chama hicho kinaendelea kuwa na ushawishi baada ya uchaguzi ujao.
Mwanasiasa Chapia Chapia, ambaye pia ni mhamasishaji wa chama mashinani, alitaka uongozi kuhakikisha makubaliano ya kisiasa kati ya UDA na ODM hayaathiri ukuaji wa vyama vingine.