Siasa

Mpango wa Gachagua Mlima Kenya waanza kuyumba

Na JUSTUS OCHIENG November 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

JUHUDI za aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua za kuunganisha eneo la Mlima Kenya chini ya chama chake cha Democracy for the Citizens (DCP) zinakabiliwa na changamoto mpya huku wanasiasa wengine wakitafuta nafasi katika siasa za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kuibuka tena kisiasa kwa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, azma huru za Spika wa wa zamani wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na kiongozi wa Party of National Unity (PNU) Peter Munya, pamoja na kurejea kwa Martha Karua katika shughuli za upinzani, kunatishia kuvuruga mipango ya Bw Gachagua.

Wachanganuzi wanasema suala kubwa si iwapo tu Gachagua atashiriki uchaguzi kutokana na changamoto zake za kisheria, bali pia nani atawakilisha Mlima Kenya katika tiketi ya urais ya upinzani na nafasi ambayo eneo hilo litapata katika serikali ijayo.

Mchambuzi Geoffrey Mboya anasema Gachagua anakabiliwa na mtihani wa kudumisha ushawishi aliojenga bila kuruhusu wapinzani wake wa kisiasa kuchukua nafasi ya kuongoza eneo hilo.

“Mtihani si iwapo Gachagua anaweza kushinda changamoto zake za kisheria na kuwania uchaguzi tu. Ni kuhusu nani anaweza kumuunga mkono, namna atakavyohakikisha eneo hilo linapata nafasi katika serikali, upinzani ukishinda na iwapo anaweza kuwazuia wapinzani wapya kuchukua ushawishi aliojenga,” anasema.

Mojawapo ya changamoto zake ni kutokuwa na uhakika kuhusu hatma ya azma yake ya kuwania urais. Mahakama Kuu ilikataa kubatilisha uamuzi wa Seneti uliomuondoa mamlakani, hivyo kumlazimu kukata rufaa.

Wakili Chris Omore anasema hali hiyo inatatiza juhudi zake za kujitambulisha kama mgombeaji urais kutoka Mlima Kenya, na huenda ikaeleza kwa nini anataka kuchelewesha kutajwa kwa mgombeaji mmoja wa upinzani hadi rufaa yake iamuliwe.

Gachagua sasa ana chaguo gumu: kuongoza tiketi ya upinzani, kumuunga mkono mgombeaji kutoka eneo jingine au kujadiliana ili mwanasiasa mwingine wa Mlima Kenya apate nafasi ya juu serikalini.

Wakati huohuo, Bw Nyoro ameanzisha chama cha People’s Party of Kenya na kuungana na Karua pamoja na mgombeaji wa urais wa Jubilee Fred Matiang’i katika mikutano ya kuimarisha upinzani.

Mkutano wao wa hivi karibuni ulifanyika jana Limuru, Kaunti ya Kiambu.

Muungano huo unachipuza mrengo mwingine wa kisiasa unaoweza kupunguza ushawishi wa DCP katika eneo la Mlima Kenya.

Matiang’i amepinga siasa zinazotegemea kugawa jamii kwa msingi wa kabila, akisema mgombeaji wa urais anapaswa kuchaguliwa na wapigakura badala ya viongozi kugawana nyadhifa kulingana na jamii zao.

“Uongozi na mustakabali wa nchi yetu haupaswi kuamuliwa kupitia mgawanyiko wa kikabila,” akasema.

Karua naye ana uzito wake kisiasa. Alikuwa mgombeaji mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022, akiwa na chama chake, wafuasi na uzoefu wa kuwania urais.

Mboya anasema uwepo wake unamaanisha siasa za Mlima Kenya haziwezi kupunguzwa kuwa ushindani kati ya Gachagua na Naibu Rais Kithure Kindiki.

Kindiki, ambaye yuko katika serikali ya Rais William Ruto, anatumia nafasi yake kupigia debe eneo hilo ndani ya Kenya Kwanza.

Ameonya kuwa Mlima Kenya unaweza kupoteza nafasi yake iwapo utaingia katika muungano wa upinzani bila kuwa na mgombeaji mkuu kutoka eneo hilo.

“Baada ya William Ruto, sisi ndio tunafuata. Katika upande mwingine, itachukua miaka 200 kabla zamu yetu kufika,” alisema.

Muturi na Munya wamekataa shinikizo la vyama vidogo vya Mlima Kenya kuvunjwa na kujiunga na DCP, wakisisitiza kuwa ushirikiano haupaswi kumaanisha kusalimisha vyama vyao.

Munya pia amepinga mazungumzo ya muungano kufanyika nyumbani kwa Gachagua, Wamunyoro, akipendelea jukwaa lisiloegemea upande wowote.

Muturi ameshiriki kampeni ya Ukombozi pamoja na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa katika kaunti za Migori na Homa Bay, ishara kwamba anachunguza miungano mingine nje ya DCP.

Kwa upande mwingine, Gachagua amekutana na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu katika Wamunyoro, siku chache baada ya kumkaribisha Kalonzo.

Hatua hiyo imetafsiriwa kuwa juhudi za kupanua ushawishi wake katika Ukambani, eneo ambalo limekuwa ngome ya Wiper.

Gachagua amesema yuko tayari kumuunga mkono atakayeshinda tiketi ya urais ya upinzani, na hata amedokeza kuwa anaweza kuwa naibu wa kiongozi wa Linda Mwananchi Movement Edwin Sifuna iwapo hesabu za kisiasa zitaelekeza hivyo.