Habari

Madiwani wapitisha hoja ya kumwondoa ofisini Gavana Samboja

October 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LUCY MKANYIKA na CHARLES WASONGA

HUENDA Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja atafutwa kazi ikiwa Seneti litaidhinisha hoja ya kumwondoa ofisini iliyopitishwa na madiwani wa kaunti yake Jumatano.

Jumla ya madiwani 30 kati ya madiwano 35 wa kaunti hiyo waliunga mkono hoja hiyo iliyodhaminiwa na naibu kiongozi wa wengi, diwani Haris Keke.

Miongoni mwa sababu za kumwondoa gavana Samboja afisini kulingana na hoja ya diwani huyo wa wadi ya Rong’e ni kwamba amefeli kuidhinisha bajeti ya kaunti hiyo kutekeleza miradi bila kushirikisha maoni ya umma.

Vilevile, madiwani hao wanadai kuwa serikali ya Gavana Samboja imefeli kuwasilisha michango ya wafanyakazi wa kaunti hiyo katika hazina za kulinda masilahi yao.

“Licha ya serikali ya Kaunti ya Taita Taveta kukata michango ya wafanyakazi – Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) na Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) – pesa hizo hazijakuwa zikiwasilishwa katika taasisi hizo. Hii ni kinyume cha sheria na inayaweka masilahi ya wafanyakazi hatarini,” akasema Diwani wa Wadi ya Sagale Godwin Kilele akiunga mkono mjadala kuhusu hoja hiyo.

Hadaa

Madiwani hao pia walimsuta Bw Samboja kwa kile walidai ni kuwahadaa wakazi wa kaunti ya Taita Taveta alipokusanya sahihi zao 52,000 kwa kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa kuvunja kaunti hiyo.

“Mpaka sasa sahihi hizo hazijawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta jinsi alivyoahidi; ishara kwamba gavana Samboja alikuwa akiwachezea shere wananchi kwa maana ya wakazi wa kaunti hii. Isitoshe, madai kwamba tulijitengea Sh840 milioni kwenye bajeti hayana msingi wowote,” akasema Bw Kilele.

Hoja hiyo sasa itawasilishwa kwa Bunge la Seneti ambalo litateua kamati ya maseneta 11 kuchunguza uhalali wa madai ya madiwani hao ili kuyaidhinisha au kuyatupilia mbali.