Habari

Mafuriko ya ghafla yahangaisha wakazi eneo la kaskazini mwa Bonde la Ufa

Na BARNABAS BII August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA kadhaa zimeachwa bila makao katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa kufuatia mafuriko ya ghafla yaliyosababishwa na mvua kubwa, huku ikibainika kuwa serikali za kaunti hazina uwezo wa kukabiliana ipasavyo na majanga.

Katika Kaunti ya Turkana pekee, zaidi ya watu 100 wameachwa bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.

Mali ya thamani isiyojulikana imeharibiwa, huku barabara nyingi katika kaunti za Elgeyo Marakwet, Baringo, Trans Nzoia na Nandi zikiwa hazipitiki kutokana na athari za mvua kubwa inayoharibu miundomsingi na mimea.

Ripoti ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya inaonyesha kuwa watoto wawili hawajulikani walipo na zaidi ya watu 100 wanalala nje kwenye baridi katika eneo la Kapedo, mpakani mwa Turkana na Baringo, baada ya mito ya msimu kuvunja kingo zake.

“Operesheni ya kuwasaka watoto waliopotea inaendelea huku timu ya dharura ikitumwa kufanya tathmini ya hali ya kibinadamu kwa familia zilizoathirika,” alisema Meneja wa Shirika la Msalaba Mwekundu anayesimamia eneo la North Rift, Bw Oscar Okumu.

Alifichua kuwa familia 49 zimehamishwa katika Kaunti ya Trans Nzoia kutokana na mafuriko, huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ikitoa onyo la mvua kubwa inayoendelea kunyesha maeneo mengi ya nchi.

“Tunaongeza uwezo wetu wa kukabiliana na athari za mvua kubwa katika kaunti ambazo huenda zikakumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi,” alisema Bw Okumu.

Miongoni mwa kaunti zinazolengwa ni Elgeyo Marakwet, Turkana, Pokot Magharibi, Nandi, Trans Nzoia na Bungoma.

Hata hivyo, inabainika kuwa kaunti nyingi hazina vifaa na rasilmali za kukabiliana na majanga kama mafuriko na maporomoko ya ardhi kwa kukosa vifaa vinavyofaa na wafanyakazi walio na mafunzo ya kushughulikia hali hiyo.

Aidha, hazina Kamati za Dharura na Maandalizi ya Kukabiliana na Majanga, wakati ambapo Idara ya Hali ya Hewa imeonya kuhusu kuendelea kwa mvua kubwa.