Habari

Magavana Pwani watolewa jasho washindani wakiapa kuwafanya wa muhula mmoja

Na WINNIE ATIENO August 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAGAVANA wanne wanaohudumu hatamu zao za kwanza katika kaunti za Pwani, wanakumbwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wanaomezea mate viti hivyo tukielekea mwaka wa 2027.

Washindani wa magavana Bi Fatuma Achani (Kwale), Bw Abdulswamad Nassir (Mombasa), Bw Andrew Mwadime (Taita Taveta), na Bw Gideon Mung’aro (Kilifi), wameanza kukosoa vikali utendakazi wao wakisema wameshindwa kutatua changamoto zinazokabili kaunti hizo nne.

Katika Kaunti ya Kilifi, Bw Mung’aro amesema yuko tayari kupambana na aliyekuwa Waziri wa Jinsia Bi Aisha Jumwa, ambaye amekuwa akikosoa uongozi wake.

“Nimekuwa nikinyamaza lakini sasa nimechoka na hizi siasa zako, sasa acha tupambane. Nitakuonyesha kivumbi kama vile nilikuonyesha wakati wa uchaguzi mkuu uliopita,” alionya Gavana Mung’aro.

Katika Kaunti ya Mombasa, Bw Nassir anaendelea kukosolewa na Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, aliyekuwa Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, na mbunge wa zamani wa Nyali, Bw Awiti Bolo, kwa kutowekeza kwenye miradi ya maendeleo.

Katika Kaunti ya Kwale, Bi Achani naye asema kuna njama ya mabwanyenye ambao wanapania kufadhili wapinzani wake ili kumuondoa mamlakani.

Aidha, Bi Achani anadai njama hiyo ilipangwa kutokana na juhudi zake za kupambana na wanyakuzi wa ardhi.

Mpinzani wake mkubwa, Prof Hamadi Boga (ODM), amekuwa akifanya mikutano na vijana akiwahimiza kudumisha amani, kujihusisha na maswala ya elimu ya kiufundi hasa kilimo ili kupata mapato badala ya kukaa maskani.

Prof Boga pia amekuwa akimshtumu Gavana Achani kwa kudorora kwa sekta ya afya na utovu wa usalama.

Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Bw Chirau Ali Mwakwere, pia amekuwa akimshtumu Gavana Achani, akisema ameshindwa kupambana na unyakuzi wa adhi na kuwaacha wakazi masquota.

Kwingineko katika Kaunti ya Taita Taveta, Bw Mwadime anatolewa kijasho na wanasiasa kadha wakiwemo Mbunge wa Wundanyi Bw Danson Mwashako, wa chama cha Wiper Patriotic Front, aliyekuwa Gavana wa kaunti hiyo Bw Granton Samboja, Seneta Jones Mwaruma, miongoni mwa wengine.

Wapinzani wanataka magavana hao waeleze miradi ya maendeleo waliyoanzisha tangu wachukue mamlaka baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Magavana wa Kaunti za Lamu na Tana River, Bw Issa Timamy na Bw Dhadho Godhana, wanatumikia hatamu zao za pili ambazo ni za mwisho kikatiba. Bw Timamy aliashiria analenga kuelekea kwa siasa za kitaifa huku Bw Godhana akilenga useneta.