Magenge ya vijana Murang'a yasababisha changamoto kuu za kiusalama
Na MWANGI MUIRURI
KWA muda sasa wa takriban miaka minne mfululizo, miji kadha ya kaunti ya Murang’a imekuwa ikitatizwa na magenge ya vijana wadogo ambao hujifahamisha waziwazi kama makundi ya kijambazi.
Makundi hayo ni pamoja na Gaza, Mungiki, Nja Nene, Njata, Usiku Sacco na 42 Brothers.
Kundi lingine ambalo limechipuka linaitwa Amba Nyambure; yaani, lugha ya Gikuyu linalomaanisha “kujihusisha na ubomozi.”
Ni hali ambayo imekumba kwa kiwango kikuu kaunti ndogo za Maragua, Kigumo na Kiharu miji ya Mukuyu na mji wa Murang’a sawia na mtaa wa Mjini katika Kaunti ndogo ya Kiharu, PCEA madukani katika Kaunti ya Kigumo na Makuyu katika kaunti ndogo ya Maragua.
Mjini Kenol pia kuna makundi kadhaa chini ya mpangilio huu, hali ambayo imesababisha taharuki kuu katika eneo hilo kuhusu usalama.
Wenyeji katika mitaa mbalimbali wamekuwa wakitisha kuwajibikia usalama wao ikiwa maafisa wa kiusalama watazidi kuzembea katika jukumu la kudhalalisha makundi haya.
Lakini afisa mmoja wa polisi aliambia Taifa Leo kuwa hili ni suala nyeti sana.
“Baadhi ya hawa vijana tunawajua na tunafahamu jinsi wanahangaisha wenyeji, lakini hakuna raia ambao hukubali kuwa mashahidi ili tuwakamate wahalifu hawa na tuwafungulie mashtaka,” alisema afisa huyo ambaye hatumtaji.
Afisa huyo anateta kuwa hawawezi wakajihami kwa bunduki na risasi waanze kuwasakama wakiwaangamiza.
“Kuna shida kuu kuhusu usalama wa eneo hili na cha muhimu, ni nafasi za kazi ziundwe ili wengi wajipe ajira halali. Ukosefu wa ajira eneo hili la Murang’a unasikitisha na hatuwezi kutumiwa kuua waathiriwa wa umasikini,” akasema.
Kamishna wa Murang’a, Mohammed Barre anakiri kuwa kero hiyo ya kundi hilo la magenge ya vijana imejitandaza katika maeneo ya Kiawamburi, Maragi na Mukuyu na ambapo kumekuwa na taharuki kati ya wenyeji na magenge hayo wakipanga njama za kisasi.
Amesema kuwa habari kuhusu hali hiyo hatari zilifikia idara ya polisi “na ndipo niliandaa mkutano wa dharura na kuwaagiza maafisa wangu waingie nyanjani na wawasake wafuasi wa genge hilo kwa nia ya kuangamiza mtandao huo.”
“Amri hiyo inazidi kutekelezwa na hadi sasa kuna wafuasi sugu wa magenge hayo ambao wametiwa mbaroni na kushtakiwa,” akasema.
Maafisa wa kiusalama wanasema inaonekana vijana wengi ambao wanafurushwa mtaani Kayole katika msako mkali dhidi ya magenge ya vijana wanatorokea Murang’a.
Akaonya Bw Barre: “Ikiwa Nairobi kuna joto la polisi, hapa Murang’a ndio moto unaoleta joto hilo umewashwa. Hakuna pa kujificha hapa Murang’a.”
Alisema kuwa hofu yake kuu ni kuwa “wote wa washukiwa hao ni watundu wa kawaida ambao walikataa masomo na kuamua kusaka utajiri wa haraka. Tamaa ni mbaya, na tamaa huua. Tuna dawa ya kila aina kwa wale wakaidi wa dhati na ambao watanaswa wakiwa wamejihami na wakihatarisha usalama wa eneo hili.”
Kamanda wa polisi wa kaunti Josephat Kinyua anasema idara ya polisi imepata habari kuwa genge hilo huwa limejihami kwa visu nyakati za usiku na kazi yao ni kuvizia wateja na wapitanjia katika Kaunti hiyo na hatimaye kuwapora na pia kutoza biashara ushuru haramu.
Amesema kuwa utathimini wa kina kuhusu genge hilo ni kwamba lina utendakazi sawa na ule wa Mungiki.
“Kwa msingi huo, hii ni amri kwa maafisa wote wa polisi wanaohudumu katika eneo hili chini ya amri ya makao makuu ya polisi Murang’a ambapo mimi ndiye kamanda kuwa genge hilo lisakamwe kwa nguvu zote za sheria,” akasema.
Alionya vikali maafisa hao dhidi ya kutepetea kazini akisema kuwa “amri zote za kuwajibika na kuangazia kikosi chetu kama kilicho na uwezo na nia wa kutekeleza majukumu yake rasmi lazima zitimizwe pasipo njia za mkato.”
Alisema kuwa “raha ya afisa wa polisi ni kuvuna manufaa ya juhudi zake za kuhakikisha usalama umedumishwa na wananchi walio chini ya tegemeo la kulindwa na serikali wanaendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa pasipo kutatizika.”