Habari

Magenge yamerejea – Kamishna

October 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

WAKUU wa usalama mjini Mombasa wameeleza hali ya wasiwasi kufuatia kuzuka upya kwa magenge ya ujambazi mjini humu tangu kulegezwa kwa marufuku ya kutotoka nje usiku.

Walisema kuwa visa vya uhalifu mjini humo vilikuwa vimeenda chini kufuatia masharti ya kudhibiti ugonjwa wa Covid 19 kama marufuku ya kutoka nje usiku.

Muda wa kafyu ulipunguzwa ambapo sasa ni kuanzia saa tano usiku hadi saa kumi alfajiri.

“Visa vya uhalifu katika mji huu vilikuwa vimepungua maradufu lakini tangu kulegezwa kwa kafyu tumeona visa hivi vikizuka upya. Siku chache zilizopita kuna vijana waliokata watu kwa mapanga eneo la Likoni,” akasema kamishna wa Kaunti ya Mombasa Bw Gilbert Kitiyo.

Alisema mwishoni mwa juma lililopita genge la majambazi lilivamia wakazi eneobunge la Likoni ambapo washukiwa wawili waliuawa.

Aliwahimiza wazee wa mtaa, machifu, na viongozi wa kidini kuhakikisha wanashirikiana na maafisa wa usalama kuona kwamba visa hivyo havikithiri.

“Tunawaomba viongozi mashinani kutoruhusu visa hivi kurudi. Kuona kundi la vijana 30 na mapanga wakitembea mtaani inamaanisha kuwa wakazi wamekubali hao vijana wawatawale,” akasema.

Aidha, aliwaonya wanaojihusisha na uhalifu kuwa maisha yao yatakuwa mafupi.

“Tunataka hawa vijana kujua kuwa tutakapowakamata hakuna kwenda kortini, wanaenda korti kufanya nini wakati wanaua watu,” akasema.

Wakati huo huo, alisema idara ya usalama itashirikiana na wakuu wa mahakama kuangamiza makundi yanayonyakua mashamba ya watu.

Alisema wavamizi hao wamekithiri katika maeneo ya Likoni, Nyali na Kisauni ambapo wanapovamia, hugawana na kuuza ardhi za watu.

“Hawa watu ni wajanja ambao wanapovamia, wanakimbia mahakamani kuwazuia wamiliki halisi kuwafurusha kisha huanza kugawanya na kuuza ardhi isiyo yao,” akasema Bw Kitiyo.

Mkuu wa polisi katika eneo hilo Bw Julius Kiragu alisema, visa vya wanyakuzi hao sasa vimeshinda vile vya wahalifu wa mapanga ambavyo vilikuwa vinawahangaisha wakazi katika eneo hilo.

“Kitu kinachotusumbua sasa ni wanyakuzi wa ardhi ambao wanavamia ardhi za watu kisha kuanza kuzigawa na kuuza,” akasema Bw Kiragu.

Alieleza kuwa wanyakuzi hao hugawanya ardhi hizo na kuwauzia Wakenya wasio na habari kwa bei ya kutupa.

Aidha, alisema kuwa mwenye ardhi anapogutukia na kutaka kuwafurusha, wavamizi hao hujenga makaburi bandia kisha kukimbilia kortini wakitaka amri ya kutofurushwa.

“Watu hawa hutumia njia mbali mbali kushawishi serikali. Huchimba makaburi ambayo ndani hamna kitu wakidai ni makaburi ya mababu zao kabla ya kukimbia kortini,” akasema mkuu huyo.

Alisema wanyakuzi hao hujificha nyuma ya dhuluma za ardhi na kuongeza kuwa wanapomaliza kuuza ardhi hiyo hutoka na kwenda kwingine.