Habari

Magoha afutilia mbali uteuzi wa Prof Kiama kama Naibu Chansela UoN

January 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu George Magoha amevunjilia mbali Baraza la Usimamizi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) na kubatilisha uteuzi wa Prof Stephen Gitahi Kiama kama Naibu Chansela wa chuo hicho.

Kwenye taarifa aliyotoa Ijumaa, Januari 17, 2020, Prof Magoha alisema amechukua hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa mashauriano zaidi kuhusu mchakato wa uteuzi wa Naibu Chansela mpya.

Alisema wakati huu Prof Kiama ataendelea kutekeleza majukumu yake kama Naibu Chansela anayesimamia masuala ya wafanyakazi na usimamizi.

Profesa Magoha alimteua tena Naibu Chansela anayesimamia Masuala ya Fedha Mipango na Maendeleo Profesa Isaac Meroka Mbeche kuwa kaimu Naibu Chansela wa UoN.

Mapema Januari baraza la chuo hicho chini ya uongozi wa Profesa Julia Ojiambo lilikuwa limemteua Prof Kiama kuwa Naibu Chansela kuchukua pahala pa Profesa Peter Mbithi.

“Nachukau nafasi hii kushukuru Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), wenzetu katika baraza, wizara ya elimu, jamii yote ya chuo na Chansela wetu kwa ushirikiano wao uliofanikilisha shughuli hii ya uteuzi,” Profesa Ojiambo akasema mnamo Januari 5, 2020.

Akaongeza: “Tunamshukuru Naibu Chansela mpya kwa uteuzi huu. Vilevile, tunawashukuru wote walioitikia wito wetu na kutuma maombi ya kiti hiki na kujitolea kwao kuhudumu kama Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi.”

Watu 14, miongoni wa waliotuma maombi ya kutaka cheo hicho, walihojiwa.

Miongoni mwao walikuwa Prof Benard Kimani Njoroge, Prof Solomon Igosangwa Shibairo, Prof Patricia Kameri Mbote, Prof Madara Ogot, Prof Kareithi Ruth Wanjiru Nduati, Prof Stephen Kiama Gitahi, Prof Elijah Omwenga, na Prof Mbeche.

Wale ambao hawakuorodheshwa kwa mahojiano ni pamoja na; Prof Duke Omondi Otara, Prof Maurice Amutabi, Prof Isaiah Omolo Ndiege, Prof Julius Onyango Ochuodho, Prof Collins Ogutu Miruka na Prof Shitanda Douglas.

Shughuli ya uteuzi wa Naibu Chansela iliendeshwa na PSC chini ya usimamizi wa baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi.

Prof Kiama alipaswa kuanza hatamu yake ya uongozi mara moja.

Hata hivyo, duru zimeambia ‘Taifa Leo’ kwamba uteuzi wake haukuidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta ndiposa Profesa Magoha akaubatilisha.