Habari

Magoha awaonya vikali wanaojihusisha na udanganyifu KCSE

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON AYIENDA

SERIKALI inaiangazia Kaunti ya Kisii baada ya watu 12 kukamatwa kwa kujifanya watahiniwa katika visa vinavyoorodheshwa kuwa miongoni mwa matukio ya udanganyifu katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE 2019) ambao ulianza rasmi Jumatatu.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema Jumatano kwamba wanaendelea kufuatilia habari na fununu muhimu zitakazosaidia kuwakamata washukiwa wengine wa udanganyifu katika mitihani.

Waziri huyo alikuwa akihutubu katika kituo cha mtihani wa KCSE cha Inter-City, Kaunti ya Kisii ambapo watu 12 walikamatwa kuhusiana na kujifanya watahiniwa kwa njia zisizo wazi.

Watahiniwa 16 wamekosa kufika kufanya mtihani wao baada ya kamatakamata ya Jumanne. Kituo hicho kina idadi jumla ya watahiniwa 36.

“Tumepata fununu kwamba baadhi ya wazazi wamekusanya pesa katika lengo la kuwasaidia watahiniwa kufanya udanganyifu. Ninawaonya kwamba yeyote atakayekamatwa atachukuliwa hatua kali kisheria,” amesema Magoha.

Kwa kipindi cha miaka mitatu sasa, Kisii imekuwa ikitajwatajwa kuhusiana na visa vya ukiukaji sheria na kanuni za mtihani wa uwazi.

Shule zingine ambazo zimemulikwa ni za Homa Bay na Thika, kwa mujibu wa waziri.

Wasimamizi wa vituo vya watahiniwa kufanyia mtihani watakuwa wanajiweka katika uwezekano mkubwa wa kupoteza kazi zao ikiwa maafisa wa polisi hawatakuwa katika vituo hivyo wakati mtihani ukiendelea.

Kila kituo, waziri amependekeza, ni vizuri kiwe na angalau maafisa wawili wa polisi.

Kituo cha Inter-City kinawachukua watahiniwa kutoka shule mbalimbali, lakini Magoha amesema kitatathminiwa upya na ikilazimu, huenda kikafungwa.