Magoha aweka wazi utaratibu wa kutathmini hatua za wanafunzi wa gredi ya tatu
Na LAWRENCE ONGARO
WAKENYA wamepewa hakikisho kuwa mitihani ya mwaka 2019 ya kidato cha nne na darasa la nane haitaibwa hii ikiwa ni baada ya serikali kuweka mikakati maalum.
Waziri wa Elimu, George Magoha, amesema tayari wizara yake imeweka mikakati kabambe ambapo “hakuna yeyote atapata nafasi ya kuiba mitihani ya mwaka huu wa 2019.”
Ametaja maeneo kama Homa Bay, Kisii na Rongo kama sehemu wanazomulika vilivyo na tayari wameweka mikakati inayostahili.
“Tayari nimezungumza na maafisa wangu kuona ya kwamba mitihani ya mwaka huu inaendeshwa kwa njia inayostahili bila wanafunzi kudanganywa kuwa watauziwa karatasi za mitihani kabla ya wakati wake,” amesema waziri Magoha.
Ameyasema hayo Ijumaa katika Shule ya Msingi ya JoyTown mjini Thika, alipozuru kujionea mwenyewe jinsi wanafunzi wa darasa la tatu – gredi ya tatu – wanavyopewa mafunzo ya uangalizi na tathmini ya kila mara.
Amesema hakuna mtihani wowote unaoendeshwa kwa watoto hao lakini cha muhimu ni kuona jinsi wanavyoelewa masomo wanayofunzwa darasani.
“Nyinyi waandishi wa habari mnastahili kuelezea Wakenya kuwa huo sio mtihani wanaofanyiwa wanafunzi lakini ni mchakato wa kila mara wa kutathmini jinsi mwanafunzi anavyofahamu masomo yake ili kumtayarisha vilivyo kusonga mbele kwa darasa la nne,” amefafanua Bw Magoha.
Anefafanua kuwa masomo muhimu yatakayopewa zingatio kuu ni somo la Hisabati na Kiingereza.
Amesema shule za walemavu zitatiliwa maanani zaidi kwa sababu kuna ukosefu wa walimu wa kutosha na vitabu.
“Tunataka kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki yake bila kumbagua kwa misingi ya kiafya. Kwa hivyo, kila mwalimu atekeleze wajibu wake ipasavyo,” amesema Magoha.
Katika ziara hiyo waziri huyo amepata fursa kuzunguka madarasa kadha na kuketi na wanafunzi hao wa darasa la tatu na kujionea mwenyewe jinsi wanavyosoma na kujieleza.
Alitoa amri kila mwanafunzi apate kitabu chake mwenyewe ili aweze kujifanyia kazi yake mwenyewe kwa kufuata maagizo.