Habari

Mahabusu aliyepigwa risasi akitoroka polisi atambuliwa kuwa mwanasiasa tajika Embu

Na GEORGE MUNENE August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHABUSU aliyepigwa risasi na kuuawa akiwatoroka maafisa wa usalama Kaunti ya Embu ametambuliwa kama Swaleh Abdallah Njiru, maarufu kwa jina Oswando, aliyewahi kuwania kiti cha MCA Kirimari.

Oswando, 38, aligombea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha ODM mnamo 2022.

Mwili wake ulitambuliwa na familia katika mochari ya hospitali ya rufaa ya Embu baada ya kuuawa kwa risasi Jumanne, jambo lililowaacha jamaa na marafiki wa karibu wakiwa na mshtuko mkubwa.

“Tumemuona na tumemtambua kuwa ni mtoto wetu,” alisema Bw Ismail Abdallah, kaka yake marehemu.

Oswando aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya mauaji na wizi wa kutumia nguvu alitoroka alipokuwa akirejeshwa Gereza la Embu baada ya kuhudhuria kikao cha mahakama mjini Siakago.

Alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika eneo la Gatondo alipokuwa akijaribu kutoroka.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Embu Magharibi, Vincent Kitili, Oswando alikuwa akisafirishwa pamoja na washukiwa wengine gerezani, lakini ghafla alishambulia maafisa wa usalama waliokuwa ndani ya gari hilo.

Alitoa pilipili na kuwapulizia maafisa waliokuwa ndani ya gari hilo, jambo lililosababisha hofu na vurugu.

Katika hali hiyo, aliruka nje ya gari na kukimbia.

Hata hivyo, licha ya maumivu ya macho kutokana na pilipili hiyo, mmoja wa maafisa alimkimbiza kwa ujasiri na kumwangusha kwa risasi.