Mahakama ilivyomlemea Ruto 2025
MWAKA wa 2025, serikali ya Rais William Ruto iliendelea kukumbana na misukosuko ya kisheria baada ya mahakama kubatilisha maagizo na kanuni kadhaa ya serikali.
Maamuzi hayo, yaliyohusu mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mageuzi katika sekta ya madini, mashirika ya umma na kanuni za utumishi wa umma, yalionyesha ukiukaji wa Katiba na ukosefu wa ushirikishaji wa umma.
Moja ya hukumu muhimu ilihusu jaribio la serikali kupunguza mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Mwanasheria Mkuu kuhusu usimamizi wa wafanyakazi katika mashirika ya umma na vyuo vikuu vya umma.
Mnamo Julai 2023, Kamati ya Ushauri wa Mashirika ya Umma (SCAC), ikiungwa mkono na AG, ilitoa ilani iliyolenga kuondoa mashirika ya umma chini ya usimamizi wa PSC, ikidai kuwa hayamo katika “utumishi wa umma”.
Hata hivyo, Mahakama Kuu iliamua kuwa hatua hiyo ilikuwa kinyume cha Katiba, ikisema AG na SCAC walitwaa mamlaka ya PSC yaliyolindwa na Katiba.
Mahakama ilisema ushauri wa AG ulikiuka Kifungu cha 234 cha Katiba, kinachotoa mamlaka ya kipekee kwa PSC kusimamia masuala ya wafanyakazi katika utumishi wa umma.
Uamuzi huo pia ulifafanua kuwa mashirika ya umma na vyuo vikuu vya umma ni sehemu ya utumishi wa umma kama inavyofafanuliwa katika Kifungu cha 260 cha Katiba.
Kesi hiyo iliwasilishwa na mwanaharakati John Githongo na Katiba Institute, waliodai kuwa maagizo ya AG yalidhoofisha Katiba. Mahakama ilirejesha uwazi kwa kusisitiza kuwa mashirika ya umma lazima yatii kanuni za PSC.
Katika uamuzi mwingine, mahakama ilibatilisha kuanzishwa kwa jopo la fidia kwa waathiriwa wa ghasia za maandamano. Mahakama ilisema jukumu hilo liko chini ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR). Jopo hilo la wanachama 18, likiongozwa na Profesa Makau Mutua, lilitangazwa Agosti 25 kupitia gazeti rasmi la serikali.
Mahakama ilisema kuwa ingawa Rais ana wajibu wa kulinda haki za binadamu, hana mamlaka ya kuunda jopo hilo peke yake bila kufuata Katiba.
Mahakama pia ilibatilisha miongozo iliyotolewa na Rais Ruto Juni 2024, iliyolenga kutoa mamlaka kwa SCAC na Hazina ya Kitaifa kusimamia majukumu ya PSC na Tume ya Mishahara (SRC).
Mahakama ilisema miongozo hiyo ilikuwa kinyume cha Katiba kwa kuwa ilinyakua majukumu ya taasisi huru.
Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) kilipinga miongozo hiyo, kikisema ilikuwa jaribio la kuanzisha utumishi wa umma sambamba chini ya afisi ya Rais. Mahakama ilikubaliana na hoja hiyo.
Serikali pia ilipata pigo baada ya Mahakama Kuu kubatilisha Kanuni za Madini za 2024, zilizoongeza ada na tozo za leseni. Mahakama ilisema kanuni hizo zilikiuka kanuni ya ushirikishaji wa umma chini ya Kifungu cha 10 cha Katiba.
Kanuni za kampuni za kibinfsi za Usalama za 2019 pia zilifutiliwa mbali, mahakama ikisema hazikupitia ushirikishaji wa umma ipasavyo licha ya serikali kujaribu kuzitekeleza tena.
Mnamo Aprili 2024, Mahakama Kuu ilibatilisha agizo la serikali lililowataka wazazi kulipa ada za shule kupitia jukwaa la eCitizen. Mahakama ilisema agizo hilo lilikuwa la kibaguzi na lilitekelezwa bila ushirikishaji wa umma.
Mahakama ya Rufaa ilithibitisha uamuzi huo.
Mahakama pia ilibatilisha agizo lililotaka matangazo ya serikali kutolewa pekee kupitia KBC, ikisema lilikiuka sheria za ununuzi na kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa jumla, maamuzi haya yalisisitiza umuhimu wa kuzingatia Katiba, kuheshimu uhuru wa taasisi huru na kuhakikisha ushirikishaji wa umma katika utungaji wa sera nchini Kenya.