Mahakama yaagiza IEBC ianze upya mchakato wa kutafuta Afisa Mkuu Mtendaji
Na WALTER MENYA
KWA mara ya pili katika kipindi cha miezi saba, uteuzi wa atakayekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) umesitishwa na mahakama ya kushughulikia masuala ya wafanyakazi baada ya kubainika tume haikuzingatia sheria.
Mahakama hiyo, ELRC, Ijumaa imekubali malalamiko ya Chama cha Mawakili kilichoitaka kuiagiza IEBC kusitisha mchakato wa kuwahoji watu 10 walioteuliwa kwa ajili ya wadhifa huo ambao zamani ulishikiliwa na Ezra Chiloba lakini akatimuliwa kazini.
Katika malalamishi hayo nambari 104 ya mwaka 2019, Chama cha Mawakili, kinasema IEBC miongoni mwa dosari zingine, haikuteua shirika la masuala ya wafanyakazi kusimamia shughuli ya uteuzi kuanzia kwa wanaotuma maombi.
Pia kuna malalamiko kwamba sekritarieti ya tume ndiyo ilikuwa ikipokea na kutayarisha orodha ya watuma maombi, wakati ambapo kaimu Afisa Mkuu Mtendaji, Marjan Hussein, naye alikuwa ni mmoja wa waliotuma maombi na hivyo kuchangia mgongano wa kimaslahi.
Kando na hayo, kulikuwa na hali ya utata kampuni ya Alpex Consulting Africa Limited (ACAL) ilipokataa mkataba, siku chache tu kabla ya orodha kuchapishwa Juni 13.
ACAL ilisema “tume imekosa kutimiza vigezo na inaweza ikatuweka katika hali mbaya ya kuonekana kutofuata sheria.”
Mnamo Mei 20, 2019, Jaji Hellen Wasilwa katika uamuzi wake alisema IEBC ilichapisha nafasi ya kazi ya Afisa Mkuu Mtendaji bila kufuata sheria.
Ni katika kesi iliyoshtakiwa na Henry Mutundu, Nambari 51 ya mwaka 2019.
IEBC ilitangaza upya kazi hiyo Mei 21, 2019.