Habari

Mahakama yaagiza mabloga 3 kuomba mbunge msamaha kwa kumhusisha na mauaji

Na RICHARD MUNGUTI November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu ya Milimani imewaamuru mabloga watatu kumuomba msamaha Mbunge wa Lugari, Nabii Nabwera, kwa kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii zilizomhusisha na kupotea na kuuawa kikatili kwa mkuu wa shule ya sekondari siku tisa zilizopita.

Hata hivyo, mahakama ilikataa kuamuru mabloga hao kufuta machapisho hayo ambayo yalidai kuhusika kwa mbunge huyo na kifo cha Simon Isiaho Shange, mkuu wa Shule ya Upili ya Munyuki, ambaye alipotea Novemba 3, 2025, baada ya ajali ya barabarani katika Kaunti ya Kakamega.

Mwili wa Shange ulipatikana Novemba 8, 2025, ukiwa umetupwa kwenye Mto Kipkaren, baada ya kuripotiwa kupotea kwa siku kadhaa.

Kupitia wakili wake Danstan Omari, Nabwera aliomba mahakama iamuru mabloga hao kumuomba msamaha mara moja, akisema kuwa machapisho yao yalimchafulia jina na kumdhalilisha mbele ya umma. Mbunge huyo pia anadai fidia ya Sh60 milioni 60 kutoka kwa kila mmoja kwa kumtusi na kumchafulia jina.

Mahakama ilikubali maombi hayo kuwa ya dharura na ikatoa amri kwamba mabloga hao waandike msamaha wa hadharani kwa mbunge huyo.

“Baada ya kuzingatia ushahidi uliowasilishwa na wakili Omari, mahakama imebaini kuwa kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha msingi wa kutoa maagizo yaliyoombwa,” alisema Jaji katika uamuzi wake.

Mahakama pia ilikubaliana na hoja ya kwamba kuna ongezeko la ukiukaji wa sheria za matumizi mabaya ya kompyuta na uhalifu wa mtandaoni, hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Wanaoshitakiwa katika kesi hiyo ni Peter Amunga, George Opunga Tamata, na Simon Asievela.

Katika kesi hiyo, Nabwera anaitaka mahakama iamuru washtakiwa kufuta na kuondoa machapisho yote ya uongo, ya chuki na ya kumdhalilisha yaliyosambazwa mtandaoni.

Anasema mabloga hao hawakuwahi kumtafuta au kuomba maelezo kutoka kwake kuhusu kisa cha mwalimu huyo aliyepotea baada ya ajali.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mwili wa marehemu Shange ulipatikana na majeraha yasiyofanana na ajali ya barabarani, jambo lililopelekea kufunguliwa kwa uchunguzi wa jinai katika Kaunti ya Kakamega