Habari

Mahakama yaagiza washukiwa wa mauaji na ulaji wa binadamu wathibitishwe umri

Na EVANS JAOLA July 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Kitale Jumatatu iliamrisha umri wa washukiwa wa mauaji na ulaji wa nyama ya binadamu katika eneo la Kapenguria Kaunti ya Pokot Magharibi udhibitishwe.

Korti ilisema washukiwa hao miongoni mwa watoto sita hawawezi kushtakiwa hadi ifahamike wa umri miaka ngapi.

Washukiwa hao ambao wana asili ya Uganda walikamatwa kwa tuhuma ya kula nyama ya binadamu. Kortini, upande wa mashtaka ulikuwa umeomba uruhusiwe kuwazuilia kwa siku 30 ili kukamilisha uchunguzi.

Mbele ya Hakimu Mkuu Samuel Mokua, washukiwa hao walidai wamekuwa wakitekeleza mauaji kisha kula nyama ya binadamu.

Afisa wa uchunguzi Edward Ndem aliomba mahakama iwaruhusu wazuilie washukiwa hao katika kituo cha polisi cha Kitale akisema wamekuwa wakikabiliwa na uadui kutoka kwa umma Kapenguria.

Wananchi wenye ghadhabu walikuwa wakiwataka polisi wawaachie washukiwa hao ili wawaadhibu.

Mahakama iliridhia ombi hilo na kuwaomba washukiwa hao sita wafikishwe katika kituo cha afya cha umma kisha wazuiliwe kwenye kituo cha polisi cha Kitale.

Wanatarajiwa kurejeshwa kortini mnamo Julai 9 kwa mwelekeo zaidi kisha Julai 21 ambapo kesi yao itatajwa.

Washukiwa hao hawakuruhusiwa kukubali au kukanusha mashtaka hadi uchunguzi kuhusu kesi hiyo ukamilike.

Baada ya kukamatwa kwao mnamo Jumamosi, makachero waliarifu kuwa umma ulivamia nyumba zao na kuziteketeza. Pia kulikuwa na maandamamo ya umma yaliyosababisha barabara ya Kitale-Lodwar ifungwe katika eneo la Chesta.