Mahakama yaiamuru serikali imlipe wakili Nelson Havi Sh5.2 milioni
MAHAKAMA Kuu imeamuru Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Afisi ya Mwanasheria Mkuu zimlipe wakili Nelson Havi Sh5.2 milioni kwa kuhujumu haki zake za kikatiba alipokamatwa na kuzuiwa 2021.
Pesa hizo zinajumuisha Sh5 milioni za kufidia hasara aliyopata na riba ya kima cha Sh237,808.
Hii ni baada ya asasi hizo kufeli kuzingatia uamuzi wa mahakama hiyo uliotolewa 2023 kwamba Havi alikamatwa kinyume cha sheria.
Kesi hiyo inatokana na kisa ambapo Bw Havi, ambaye ni Rais wa zamani wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK), alikamatwa mnamo Julai 13, 2021 kwa madai ya kumdhulumu Mercy Kalondu Wambua.
Wakati huo, Bi Wambua alikuwa akihudumu kama Afisi Mkuu Mtendaji wa LSK.Wakati huu, Bi Wambua anahudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kupokea Malalamishi kutoka kwa Umma (almaarufu, Ombudsman) Katika kesi yake, Bw Havi alisema uchunguzi wa DCI na hatimaye kukamatwa kwake kulihujumu haki zake zinazolindwa chini ya vipengele vya 27 (kuhusu usawa), 28 (kuhusu utu), 29 (kutozuiliwa kiholela) na 47 (kuhusu kutendewa haki) vya Katiba.
Mnamo Desemba 2023, Mahakama Kuu ilikubaliana na Havi na kuamua kwamba kukamatwa kwake kulifanywa kinyume cha Katiba na ikaamuru afidiwe Sh5 milioni.Uamuzi huo pia uliharamisha uchunguzi dhidi yake uliutaja kama “usio na msingi”.
Isitoshe, mahakama ilisema kuwa kukamatwa kwa Bw Havi, kinyume cha sheria kuliathiri utekelezaji wa majukumu yake kama wakili na Rais wa LSK kulingana na kanuni zilizowekwa.
Lakini mawakili wa Havi walisema, hata baada ya wao kuwasilisha nakala ya uamuzi wa mahakama kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu, serikali ilifeli kulipa pesa hizo.
Hii ilimlazimisha Bw Havi kuwasilisha ombi mahakamani la kutaka serikali ilazimishwe kulipa pesa hizo.
“Mshtakiwa amekata kulipa pesa hizo licha ya kupokezwa agizo la mahakama lililotoa maelezo kuhusu malipo hayo,” mawakili wa Havi wakisema.
Jana, Mahakama Kuu ilisema kuwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu sharti itii maagizo ya Mahakama; sawa na afisi ya DCI.
Katika uamuzi wake, mahakama ilisisitiza kuwa maafisa wa umma sharti watii maagiza ya mahakama ili kujenga imani ya umma kwa mfumo wa haki.