Habari

Mahakama yakubali Philip Murgor kumtetea Sarah Wairimu Kamotho

October 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA imekubali wakili Philip Murgor kumtetea Sarah Wairimu Kamotho anayekabiliwa na tuhuma za mauaji ya mumewe, bwanyenye Tob Cohen ikisema hakuna mgongano wa kimasilahi.

Uamuzi umetolewa na Jaji Stella Mutuku.

Upande wa familia ya Cohen ulikuwa umewasilisha ombi mahakamani ukitaka Murgor ajiondoe, ukisema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ilikuwa haijaondoa jina la Murgor kama kiongozi wa mashtaka.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) naye alikuwa ameambia mahakama kuu Jumanne kwamba kuteuliwa kwa Philip Murgor kuwa kiongozi wa mashtaka hakujatenguliwa.

“Tungali kwenye mchakato wa kutengua kuteuliwa kwake,” naibu DPP Catherine Mwaniki aliambia Jaji Stella Mutuku.

Kwa upande wake Murgor alisema jinsi ambavyo Kamotho ameshughulikiwa na vyombo vya dola ni sawa na kufungwa hata kabla ya kupandishwa kizimbani na kufunguliwa mashtaka.

“Ni suala la uzito sana ikizingatiwa kwamba huyu ni raia ambaye amekuwa akizuiliwa yumkini siku 35,” alisema Murgor.

Murgor alisema alijiuzulu kuwa kiongozi wa mashtaka Machi 7.

Aidha, aliwasilisha barua aliomwandikia DPP Noordin Haji, akijiuzulu mara moja; akiongeza kwamba aliacha kuwa kiongozi wa mashtaka wakati huo.

Alieleza kwamba ombi lake lilikubalika na DPP mwenyewe.

Inashukiwa Cohen aliuawa Julai 19, 2019.