Habari

Mahakama yamwokoa Orwoba dhidi ya kutupwa kwenye kibaridi na UDA

Na JOSEPH WANGUI May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu jijini Nairobi jana ilisitisha kwa muda uamuzi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wa kumfukuza Seneta Maalum Gloria Orwoba kutoka chama hicho.

Jaji Lawrence Mugambi, alisitisha kufukuzwa kwa Orwoba na mpango wa kumteua mwanachama mwingine kwa kiti hicho hadi pale kesi aliyowasilisha seneta huyo itaposikilizwa na kuamuliwa.

“Kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, agizo la muda linatolewa kusitisha utekelezaji wa uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya Chama cha UDA wa Mei 16 2025 wa kumfukuza mlalamishi kama mwanachama wa chama cha UDA na seneta mteule,” lilisema agizo la Jaji Mugambi.

Mnamo Jumatatu, Mei 19, chama cha UDA kilimfukuza Orwoba kutoka chama hicho cha kisiasa kwa madai ya kushindwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu licha ya kuitwa.

Agizo la Jaji Mugambi lilijiri baada ya Spika wa Seneti kutangaza kiti cha Orwoba kuwa wazi kupitia ilani ya gazeti rasmi la serikali.