Mahakama yamzima mwalimu mwanamageuzi asikutane na Ruto
JUHUDI za mwalimu mmoja kutaka mahakama itoe agizo kwamba Rais William Ruto akutane naye kujadili mageuzi katika sekta ya elimu nchini zimefeli.
Bi Stella Nekesa, ambaye pia ni mwandishi wa vitabu, alielekea kortini akidai Dkt Ruto alikiuka Katiba, na haki zake, kwa kutompa miadi wakutane kujadili mapendekezo yake kuhusu njia za kuimarisha mfumo wa elimu nchini.
Katika uamuzi wake, Jaji Lawrence Mugambi alitupilia mbali ombi la Bi Nekesa.
Kwa mujibu wa Jaji, Rais hawezi kushtakiwa kama mtu binafsi kwani amepewa kinga kikatiba.
Jaji Mugambi alirejelea Kipengele cha 143 cha Katiba kinachomkinga Rais aliye mamlakani dhidi ya kufunguliwa mashtaka yoyote kortini.
“Mahakama ya Juu ilisema wazi kuwa “Rais au mtu anayetekeleza majukumu ya afisi ya rais” hawezi kushtakiwa akiwa afisini kuhusu masuala ya utekelezaji wa majukumu ya afisi yake. Mashtaka kama hayo sharti yaletwe kupitia afisi ya Mwanasheria Mkuu,” akasema Jaji Mugambi katika uamuzi wake aliutoa Ijumaa.
Bi Nekesa alisema mapendekezo ambayo alitaka kujadili na Rais Ruto pia yako kwenye kitabu chake chenye kichwa, ‘A complete stimulus framework proposal for the successful reformation of Africa’s (Kenya’s) education system)’.
Alidai kuwa kwa kukataa kukutana naye, Rais Ruto amewanyima Wakenya nafasi ya kufahamu yaliyomo kwenye kitabu chake.
Alisema mapendekezo hayo yangesaidia kuleta mageuzi bora kwa mfumo wa elimu nchini.
Katika kesi aliyowasilisha mnamo Desemba 2023 Bi Nekesa alidai kuwa hata rais mstaafu Uhuru Kenyatta alidinda kukutana naye.
Alisema kuwa kwa kukataa kukutana naye, marais hao wawili walikiuka haki zake za Kikatiba.
Rais Ruto alijibu kesi hiyo kupitia pingamizi iliyowasilishwa kortini na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor.