Habari

Mahakama yatupa nje kesi dhidi ya afisa anayedaiwa kushikilia kazi 10 za serikali

Na JOSEPH WANGUI February 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NI afueni kwa afisa mmoja wa ngazi za juu katika utumishi wa umma aliyeshtakiwa kwa madai ya kushikilia vyeo kadhaa kwa wakati mmoja, baada ya korti kutupa nje kesi ya kuzima mshahara wake.

Kulingana na kesi iliyowasilishwa na mtetezi wa haki za kibinadamu Dkt Magare Gikenyi, Bi Jennifer Gitiri alidaiwa kushikilia nafasi 10 tofauti za ajira katika asasi za umma.

Lakini Jaji Lawrence Mugambi aliamua kuwa kesi hiyo haina mashiko na kuitupilia mbali. Alisema Gikenyi anafaa kuwasilisha kesi yake katika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wala sio mahakamani kwani suala hilo linahusu uzingativu wa kanuni kuhusu maadili na utawala bora.

“Ni EACC iliyo na mamlaka kisheria kuhakikisha kuwa maafisa wa umma wanazingatia maadili yaliyoorodheshwa katika Sura ya Sita ya Katiba. Ni katika Tume hiyo ambapo aliyewasilisha kesi hii angepeleka malalamishi yake,” akasema Jaji Mugambi wa Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi.

Mwanaharakati Dkt Gikenyi alikuwa amedai Bi Gitiri anashikilia nyadhifa katika Baraza la Elimu ya Sheria, Baraza la Kushughulikia Masuala ya Sheria (KLRC), Mamlaka ya Kukusanya Ushuru Nchini (KRA), Shirika la Kulinda Mashahidi (WPA) na Shirika la Kulinda Waathiriwa wa Dhuluma (VPA).

Dkt Gikenyi aliongeza kuwa afisa huyo pia alishikilia nyadhifa zingine zikiwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Kutwaa Mali Iliyopatikana kwa Njia ya Ufisadi (ARA).

“Haiwezekani kwa Bi Gitiri kutoa huduma ipasavyo katika nyadhifa hizi zote kwani atalemewa na majukumu,” alieleza Dkt Gikenyi.

Alitaka korti kutoa agizo kwa ARA ikusanye pesa zote ambazo Bw Gitiri alilipwa na asasi hizo za umma ili zirejeshwe kwa Wizara ya Fedha.

Hata hivyo, katika uamuzi wake Jaji Mugambi alisema korti haina mamlaka ya kuagiza asasi za umma kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

“Kesi hii iliwasilishwa kabla ya EACC kuombwa iingilie kati suala hili, ambalo liko chini ya mamlaka yake. Hivyo, siwezi kutoa uamuzi wangu,” akasema Jaji huyo akieleza kuwa Idara ya Mahakama huwa inajizuia kuingilia masuala yanayohusu asasi zingine au mashirika ya serikali.

Akijitetea kuhusiana na kesi hiyo, Bi Gitiri, ambaye ni wakili, alisema hakuwa mfanyakazi wa kudumu wa asasi hizo za umma zilizoorodheshwa na Dkt Gikenyi.