Majabali wa KCSE 2018 watajwa
Na CHARLES WASONGA
OTIENO Irine Juliet wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Pangani, Nairobi ndiye bingwa katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka huu baada ya kujizolea alama ya ‘A’ kwa alama wastani ya 87.644.
Alifuatwa kwa karibu na Kaluma James kutoka Shule ya Upili ya Maseno aliyepata alama ya wastani ya 87.394 huku wa tatu akiwa Edwin Otieno Ouko wa Shule ya Upili ya Light Academy ambaye alijizolea alama ya 87.363.
Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu Amina Mohamed alisema yaliimarika zaidi ikizingatiwa kuwa idadi ya wanafunzi waliopata gredi ya A ilipanda hadi 315 ikilinganishwa na wanafunzi 142 mwaka jana. Mnamo 2016, ni wanafunzi 141 pekee waliopata gredi ya A.
“Ningependa kuipongeza Shule ya Upili ya Wasichana ya Pangani kwa kutoa mwanafunzi bora zaidi katika mwaka wa pili mfululizo. Pongezi zaidi Otieno Irine Juliet kwa kuibuka wa kwanza kitaifa!” akasema.
Mwaka huu, wanafunzi waliopata gredi ya C+ ya kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu ilikuwa ni 90,377 ikilinganishwa na wanafunzi 70,073 mwaka jana.
“Hii ina maana kuwa, kwa ujumla, matokeo ya mwaka huu yalikuwa bora zaidi kuliko miaka miwili iliyopita. Hii ni matunda ya mikakati murwa tulioweka kuzuia udanganyifu mwaka huu kwani wale wachache waliojaribu kutekeleza uovu walinaswa mapema,” Bi Mohamed alisema katika makao makuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Nairobi.
Waziri huyo alisema sababu nyingine iliyochangia matokeo hayo kuimarika ni kwamba, Wizara ya Elimu iliendesha vikao vya kujadili masuala ya kuimarisha viwango vya elimu katika kaunti zote 47. “Katika vikao hivyo, wawakilishi wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), Taasisi ya Kuandaa Mitaala (KICD), Chama cha Kitaifa cha Wazazi (KNPA) na KNEC walikuwepo,” akasema.
Licha ya kuzimwa kwa visa hivyo, matokeo ya wanafunzi 100 yalifutiliwa mbali huku jumla ya watu sita wakikamatwa na kupelekwa kortini kwa kujaribu kuiba mtihani huo. Matokeo ya baadhi ya shule pia yalisimamishwa kwa muda uchunguzi ukiendeshwa kuhusu uhalali wa matokeo yao.
Mwaka huu, jumla ya wanafunzi 660,204 walifanya mtihani huo wa KCSE huku 338,628 kati yao wakiwa wavulana na 321,576 wakiwa wasichana. Idadi hii inaashiria kuwa asilimia 51.29 walikuwa wavulana huku asilimia 48,71 wakiwa wavulana.
“Takwimu hizi zinaashiria kuwa kunakaribia kufikia usawa wa kijinsia katika wanafunzi wanaofanya mtihani wa KCSE. Kama taifa, tunapaswa kudumisha rekodi hiyo nzuri,” Dkt Mohamed akasema akiongeza kuwa katika kaunti 18, idadi ya watahiniwa wasichana ilizidi ile ya wavulana.
Kaunti hizo ni;Taita Taveta, Kwale, Nyandarua, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Machakos, Kitui, Meru, Makueni, Tharaka Nithi, Uasin Gishu, Nandi, Laikipia, Elgeyo Marakwet, Kakamega, Vihiga na Kisumu.
Wasichana walifanya vyema kuliko wavulana katika masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Dini ya Kikristo, Sanaa na ubinifu na Usanii wa Vyuma. Wenzao wa kiume nao walifanya vizuri katika masomo 20.
Waziri alieleza kuwa matokeo ya masomo 14 yaliimarika mwaka huu ikilinganishwa na masomo 13 mwaka jana. “Hata hivyo, masomo 12 yaliandikisha matokeo mabaya ikilinganishwa na masomo 13 mwaka jana,” akasema Dkt Mohamed.
Mwenyekiti wa Knec George Magoha alisema matokeo yalitoa picha halisi ya jinsi wanafunzi walifanya mtihani huo. Naye afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia aliwapongeza walimu waliosimamia mtihani huo katika zaidi ya vituo 10,000 kote nchini.