Habari

Majaji wakosoa sheria ya makosa ya kingono

Na JOSEPH WANGUI November 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WITO wa mageuzi ya haraka katika Sheria ya Makosa ya Kingono umeibuka upya, huku majaji nchini Kenya wakionyesha wasiwasi kuhusu namna sheria hiyo inavyowashughulikia watoto na matineja wanaohusiana kimapenzi kwa hiari.

Majaji wanasema sheria hiyo, hasa vifungu kuhusu vifungo vya lazima, imekuwa chanzo cha adhabu kali zisizo na uwiano na ukweli wa matukio, hasa inapohusu vijana wadogo wanaojaribu kuelewa uhusiano wa kimahaba.

Haya yanajiri wakati vijana watatu – wavulana wawili na msichana mmoja wenye umri wa kati ya miaka 17 na 19 – wakiwasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, wakitaka kuondolewa kwa vifungu vinavyoharamisha mahusiano ya kimapenzi baina ya vijana wadogo wanaokubaliana kwa hiari.

Wavulana hao wawili wanakabiliwa na hukumu ya lazima ya kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kubaka, chini ya Kifungu cha 8(1) na 8(3) cha Sheria ya Makosa ya Kingono. Hata hivyo, kesi hiyo imesitishwa hadi Mahakama Kuu itoe uamuzi kuhusu ombi lao.

Wakili wao anasema sheria hiyo inakiuka haki za kimsingi za vijana, ikiwemo uhuru wa faragha na utu, kwa kuwa haiwatofautishi na wakosaji wakubwa. Kesi yao inaungwa mkono na Mtandao wa Vijana wa Afrika (NAYA), unaosema adhabu kali huharibu maisha ya vijana na kukatiza masomo yao badala ya kuwasaidia kurekebisha mienendo.

Majaji kadhaa kutoka Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa wamekosoa sheria hiyo kwa kukosa utofauti kati ya watu wazima wanaonajisi na vijana wanaokubaliana kimapenzi.

Katika uamuzi wa mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ilisema: “Ni lazima sheria hii ichunguzwe upya kwa kina ili kushughulikia kesi zinazohusu vijana kwa vijana.”

Mahakama ya Machakos mnamo 2022 ilitangaza vifungo vya lazima kuwa kinyume cha katiba, ikisema vinaondoa uhuru wa majaji kutoa hukumu inayofaa kulingana na hali ya kesi. Hata hivyo, Mahakama ya Juu ilifafanua baadaye kuwa mahakama bado zina mamlaka ya kutoa hukumu kali zaidi inapobidi.

Majaji pia wameeleza wasiwasi kuhusu ubaguzi wa kijinsia katika mashtaka, kwani wavulana mara nyingi ndio wanaoshtakiwa pekee katika kesi za “kubakana kwa hiari.”

Katika kesi ya mwaka 2017, jaji mmoja wa Nairobi alihoji: “Ikiwa wavulana na wasichana wote ni chini ya miaka 18, je, wote hawajafanyiana kitendo kinyume cha sheria?”

Mahakama za Siaya na Mombasa pia zimebatilisha hukumu za kifungo kwa vijana waliopatikana na hatia za kubaka wenzao wa umri sawa, zikisema wote wanapaswa kusaidiwa, si kufungwa.

Kwa sasa, Bunge linajadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Kingono (2025) unaopendekeza vifungu vipya vya “tofauti ndogo ya umri” ili kutofautisha mahusiano ya hiari kati ya vijana na unajisi wa kweli.

Wataalamu wa sheria wanasema mfumo wa sasa “umejenga tafsiri kandamizi,” hasa kwa wavulana, na unahitaji marekebisho ili kulinda haki na utu wa watoto wote.