Majaji watatu kusikiliza rufaa kuhusu ushuru wa nyumba za bei nafuu
MZOZO kuhusu uhalali wa Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu umeingia awamu mpya baada ya Mahakama ya Rufaa kuelekeza kwamba jopo la majaji watano lisikize kesi hiyo kuanzia Januari 19, 2026.
Hatua hiyo inazua uzito mpya katika mzozo ambao unaathiri mamilioni ya wafanyakazi wanaokatwa asilimia 1.5 ya mishahara yao kwa mpango wa nyumba za bei nafuu.
Jaji Daniel Musinga, alisema Desemba 10, 2025 kwamba rufaa zilizowasilishwa na watu 42, miongoni mwao Seneta Okiya Omtatah na daktari wa upasuaji Magare Gikenyi, zinahitaji kusikilizwa kwa upana kwa sababu zinagusa masuala mazito ya kikatiba.
Walalamishi walikata Rufaa baada ya Mahakama Kuu mnamo Oktoba 22, 2024 kuamua kwamba Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu ni halali na kwamba ushuru wa asilimia 1.5 ya mshahara wa mfanyakazi ni halali unaolenga kutekeleza wajibu wa serikali kutoa makazi bora.
Mahakama Kuu ilisema kulikuwa na ushirikishaji wa umma wa kutosha na kwamba hakukuwa na ukiukaji wa haki.
Lakini Dkt Gikenyi alipinga uamuzi huo, akisema kuwa kulazimisha Wakenya wanaofanya kazi rasmi kuchangia mpango ambao hawana uhakika watanufaika nao ni hatua inayokiuka maadili na katiba.
Anasema sheria hiyo inabagua wafanyakazi wa sekta rasmi pekee huku wale wa sekta isiyo rasmi wakiachwa nje bila utaratibu wa wazi wa jinsi watakavyotozwa ushuru huo.
Dkt Gikenyi pia alipinga kifungu cha 54 cha sheria hiyo kinachoweka masharti kwa mnunuzi kuomba idhini ya Bodi ya Nyumba Nafuu kabla ya kuuza au kuhamisha nyumba aliyonunua. Anadai kuwa kipengee hicho kinakiuka haki ya kumiliki mali kwa uhuru.
Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilisema ushuru huo uliidhinishwa ipasavyo chini ya kifungu 4 cha Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu na kwamba Serikali ina mamlaka ya kutoza ushuru kama sehemu ya wajibu wa kujenga taifa.
Kwa sasa, Mahakama ya Rufaa itachunguza iwapo Mahakama Kuu ilitafsiri kwa usahihi katiba na sheria hiyo yenye utata.
Uamuzi utakaotolewa baada ya kusikizwa Januari 2026 ndio utakaoamua kama serikali itaendelea kukusanya ushuru huo au italazimika kubuni mfumo mpya—hali inayoweza kuathiri hatima ya mpango mzima wa nyumba za bei nafuu.