Majina ya wanaougua corona yatangazwe – Mbunge
Na MAUREEN ONGALA
MBUNGE wa Ganze, Teddy Mwambire anaitaka serikali iweke wazi majina ya watu walioambukizwa virusi vya corona, ili umma ujikinge mapema.
Mbunge huyo kwa sasa amejitenga kwa siku 14 baada ya kukutana na baadhi ya watu waliokaribiana na Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Bw Gideon Saburi aliyepatikana na virusi hivyo.
Bw Mwambire alisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya serikali kuwaokoa raia wake kutokana na janga hili la corona, kwa kuwa watajua kama waliwakaribia walioambukizwa, na hivyo kuchukua hatua ya kujitenga.
“Serikali inafaa kutangaza wale wamepatikana na virusi hivi ili tujue walienda wapi, walikutana na nani, siku gani ili watu hao wote wachukue hatua za kujikinga dhidi ya virusi hivi. Lazima sisi wenyewe tuchukue hatua ya kujitenga kama jukumu letu. Kama hatujui walioambukizwa, tunaweza kusambaza virusi hivi bila kujua,” akasema Bw Mwambire.
Maafisa wakuu katika Kaunti ya Kilifi akiwemo waziri anayesimamia uchukuzi, Bw Kenneth Kazungu wamejitenga.
Bw Kazungu amejitenga kwa siku 14 nyumbani kwake baada ya kukutana na dereva na walinzi wa Bw Saburi.Katika video moja iliyokuwa ikisambazwa katika mtandao wa WhatsApp, Bw Kazungu alisema kuwa amejitenga ili kuhakikisha kuwa hamweki mtu mwingine katika hatari.
“Hata kama sikukutana moja kwa moja na Naibu Gavana, nilikutana na wafanyikazi wake. Nakumbuka niliketi na mmoja katika kinyozi. Pia, walinzi wake na dereva walikutana na wafanyikazi katika idara ya uchukuzi na kuna waliofika ofisini mwangu, kikazi,” akasema Bw Kazungu.
Alisema maambukizi yako juu sana na hatua ya kujitenga itasaidia kuzuia usambaaji wa virusi hivi.
“Nimeieleza familia yangu kusimama mbali na mimi ili kujikinga,” akasema.
Hofu na wasiwasi uliwakumba wakazi wa Kilifi baada ya kusemekana kuwa watu wengi walikutana na naibu gavana huyu tangu arejee kutoka Ujerumani mnamo Machi 6.
Sammy Nyundo, ambaye ana uhusiano wa karibu sana na Bw Saburi ambaye pia amejitenga alisema kuwa serikali inaweka maisha ya Wakenya katika hatari.
“Majina ya watu walioambukizwa yawekwe wazi ili wale ambao waliwahi kukutana nao wafuatwe na kupatikana kwa urahisi,” akasema Bw Nyundo.
Alisema kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa kuwa naibu gavana huyo alikutana na watu wengi.
Inasemekana kuwa Bw Saburi alikutana na Kamishna wa Kilifi, Bw Magu Mutindika kabla ya kamishna huyo kukutana na wadogo wake.
Kulingana na mdokezi mmoja ambaye hakutaka atajwe kwa sababu ya kiusalama, watu 17 ambao walikutana na naibu gavana huyo moja kwa moja au kipitia wafanyikazi wake, walipimwa mnamo Jumatatu.