Majonzi mama aliyejinyonga, kuua watoto, wakizikwa
HUZUNI iligubika familia na waombolezaji, Kaunti ya Bomet, wakati wa mazishi ya mwanamke na watoto wake wawili kufuatia tukio la mauaji na kujitia kitanzi.
Lorna Cherono, 35, aliyekuwa akiugua matatizo ya kiakili kwa mujibu wa jamaa wa familia yake, aliwageuka na kuwaua watoto wake wawili, Abigael Chepkorir, 10, na Amos Kipchirchir,5.
Aliwabonda kwa kutumia chuma kabla ya kujinyonga kwa kamba ndani ya nyumba ya kaka yake mdogo alipokuwa ameachwa na watoto.
Wakazi katika kijiji cha Chebisian, Merigi, eneobunge la Bomet Mashariki, waliamkia tukio hilo la kushtusha Agosti 3, 2024, baada ya mtoto kupiga mayowe alipokumbana na miili iliyolowa damu ndani ya nyumba iliyoachwa wazi.
Mwanawe Cherono ambaye ni mwanafunzi wa sekondari ndiye pekee aliyenusurika katika familia hiyo kwa sababu alikuwa amesafiri Kericho tukio hilo lilipofanyika.
“Alikuwa na vipindi vya matatizo ya kiakili ambavyo amepambana navyo tangu 2015. Lakini alionekana kupata nafuu,” alisema Bw David Bett, kaka yake marehemu.
“Kabla ya kisa hicho kutendeka, dada yetu (Lorna) hakuonyesha dalili zozote za ugonjwa na hakuna chochote kilichoonyesha angefanya uovu wa kiwango hiki. Bado hatujakubali uhalisia.”
Bw Bett, ambaye tukio hilo lilifanyika nyumbani kwake, alisema mke wake alikuwa amesafiri kuwatembelea wakwe wake, kisa hicho kilipotokea na kumwacha Lorna kulinda boma.
“Siku hiyo, nilisafiri Kericho asubuhi kama kawaida yangu na kwenda moja kwa moja katika Kanisa la Merigi Seventh Day Adventist Church (SDA) kwa ushirika bila kujua yaliyofanyika nyumbani.”
Alikuwa anatumai kuungana na jamaa wa familia yake kanisani jinsi ilivyokuwa kawaida Jumamosi.
Siku moja kabla ya mkasa huo, alizungumza na marehemu dada yake ambaye hakuonyesha dalili za kuugua huku akimweleza jinsi hali ilivyo nyumbani na hata kumfahamisha kuwa ng’ombe wao mmoja alihitaji kukaguliwa na daktari wa mifugo.