HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Majonzi mtahiniwa wa KCSE akifariki ghafla baada ya karatasi mbili

Na GEORGE ODIWUOR November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA  moja katika kijiji cha Kanyaliech, eneo la Koyugi, Kaunti ya Homa Bay, imezama kwenye majonzi baada ya mwanafunzi wa Kidato cha Nne kufariki saa chache tu baada ya kufanya karatasi mbili za kwanza cha mtihani wa KCSE.
Congestina Achieng, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Alaro Central, aliaga dunia Jumatatu jioni baada ya kuugua ghafla akilalamikia maumivu makali ya kifua.
Kifo chake kiliwashtua wazazi, walimu na wakazi wa eneo hilo, kwani alikuwa ameanza safari ya mtihani wa kitaifa akiwa na matumaini ya kutimiza ndoto zake.
Babake, David Ogweno, alisema alipokea simu ya dharura kutoka kwa mkuu wa shule akimtaka afike kumchukua mwanawe baada ya kumaliza karatasi mbili za kwanza.
“Afya yake ilizorota haraka. Tulimkimbiza katika Hospitali ya Tamary, lakini kwa bahati mbaya aliaga dunia,” alisema Bw Ogweno.
Alisema familia imepitia changamoto za kifedha kumwezesha Congestina na watoto wengine kupata elimu. Bw Ogweno, ambaye hufanya kazi za vibarua, alisema mwanawe alikuwa na ndoto ya kuwa wakili ili kusaidia familia kujikwamua kutoka katika umaskini.
Mama yake, Pamela Atieno, alisema mwanawe alikuwa akiumwa tangu wiki jana, lakini alitarajia kupata nafuu na kufanya mtihani wa KCSE.
“Alilalamikia maumivu ya kifua, nikamnunulia dawa za dukani ili kupunguza maumivu na aweze kufanya mtihani. Baadaye nilipigiwa simu na kuambiwa hangeweza kuendelea,” alisema.
Walimu wake, Isaiah Opere na Austine Achina, walimtaja kama mwanafunzi mwenye nidhamu, mnyenyekevu na aliyejituma katika masomo.
Bw Opere alisema Congestina alikuwa mtulivu na mwenye tabia nzuri, ambaye hakuwahi kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu.
Kifo chake kimezima ndoto za msichana aliyetarajia kutumia elimu kujenga maisha bora, na kuacha familia yake ikiwa na majonzi makubwa.